Filamu, Dini na Mwanadamu wa Sasa-1
(last modified Wed, 23 Apr 2025 11:36:35 GMT )
Apr 23, 2025 11:36 UTC
  • Filamu, Dini na Mwanadamu wa Sasa-1

Kipindi chetu leo kitatupia jicho nafasi ya dini katika filamu na taathira zake kwa mwanadamu wa sasa.

Huenda na wewe mpenzi msikilizaji umekwishasikia au kusoma makala inayozitaja zama za sasa kuwa ni zama za “kurejea kwenye dini” au zile zinazoitaja milenia hii kuwa ni “Milenia ya Kurudi Kwenye Dini”. Mwamko na harakati mpya za dini zilipamba moto zaidi katika nchi za Magharibi mwanzoni mwa muongo wa tisini hususan mwaka wa 2000. Baadhi ya jumuiya za masuala ya kijamii huko Magharibi aidha zinaamini kwamba, kuna haja ya kutiliwa maanani misingi ya dini, maadili na masuala ya kiroho kwa ajili ya kuzuia kusambaratika kwa nchi hizo. Wimbi hilo linalowaelekeza na kuwarejesha watu kwenye dini na masuala ya kiroho linaonekana pia kwenye athari za sanaa hususan tasnia ya filamu.

Iwapo kweli tunataka kuzungumzia nafasi ya dini katika filamu za zama hizi basi hatuna budi kuashiria watu kama vile Carl Theodor Dreyer, Ingmar Bergmen, Robert Bereson na Andrei Tarkovski ambao wametengeneza filamu nyingi zenye mielekeo ya kidini katika miongo iliyopita. Baada yao na katika zama za sasa kumejitokeza watengeneza filamu wengine katika maeneo mbalimbali duniani waliotengeneza filamu nyingi katika uwanja huo.

Hebu kwanza tutupie jicho sekta ya utengenezaji filamu ya Hollywood inayozalisha zaidi ya filamu elfu moja kwa mwaka ambayo kutokana na nguvu yake kubwa imekuwa na ushawishi katika nyanja za utamaduni na filamu kwenye maeneo mablimbali duniani. Japokuwa moja ya sifa kuu za filamu za Hollywood ni hadaa, udanyifu na uchochezi, lakini filamu hizo hazikutupilia mbali kikamilifu masuala ya kidini na kiroho.

Baada ya mafanikio ya kibiashara ya filamu kama vile Ghost na Leaf of Faith, watayarishaji wa filamu za Hollywood walitambua kwamba, watazamaji wa filamu hizo wana mahitaji mengi ya kiroho ambayo hayawezi kukidhiwa kwa filamu za visa vingi vya utumiaji mabavu na zisizokuwa na mambo ya maana. Kwa msingi huo, Hollywood ilitumia mbinu zake za mara kwa mara za kuvutia na kuwashawishi watazamaji. Kwa maana kwamba, ilitumia vigezo muhimu kama vile melodrama, comedy au tamthilia ya kuchekesha, muzika na kadhalika katika kutengeneza filamu zenye mwelekeo wa kidini. Kwa mfano, katika filamu ya Ghost kumetumiwa vigezo vya filamu ya mapenzi na vitendo vya jinai kuzungumzia udaima wa roho na kubakia kwake milele ambako pia kumeashiriwa katika dini mbalimbali na kwa njia tofauti.

Baada ya mafanikio ya baadhi ya filamu hizo, masuala ya kidini na kiroho yalianza kutumiwa katika filamu nyingi za Hollywood. Tokea wakati huo filamu zilianza kuzungumzia maudhui mbalimbali kama vile kuwepo kwa Malaika wa Mungu juu ya ardhi, Shetani na wasaidizi wake katika maisha ya wanadamu na kadhalika. Hata hivyo nyingi kati ya filamu hizo zilikumbwa na wimbi la opotoshaji katika kuzungumzia masuala halisi ya kidini, na taratibu, masuala hayo yalianza kufanyiwa maskhara na istihzai. Mwenendo huo uliendelea na kufikia kiwango cha kufanyiwa stihzai na kebehi nguvu na uwezo wa Mwenyezi Mungu katika filamu ya "Bruce Almighty" iliyofungua njia pana kwa ajili ya fikra zinazopinga dini katika tasnia ya utengenezaji filamu. Filamu hiyo ilipigwa vita na wafuasi wa dini za Kiislamu na Kikristo kutokana na kupotosha masuala ya kidini.

            MUUZIKI

Katika upande mwingine ujahili wa watengenezaji filamu wa Magharibi kuhusu dini za Mwenyezi Mungu na uchache wa maarifa yao kuhusu dini zenye mashiko sahihi kama Uislamu, na vilevile woga uliozushwa na vyombo vya kipropaganda vya Magharibi kuhusu dini hizo, vimewaelekeza baadhi ya watengezaji filamu wa Hollywood katika mifumo ya kifikra isiyokuwa ya dini za Mwenyezi Mungu. Filamu za Hollywood zilianza kuzungumzia mifumo ya kidini iliyobuniwa na wanadamu kama vile Ubudha na kubuni riwaya mbalimbali kuhusu Budha na Lama. Katika uwanja huo tunaweza kuashiria filama kama vile “The Little Buddha”, “Seven Years in Tibet” na “Kundun”. Kupitia njia hiyo, baadhi ya ada na mielekeo makhsusi ya watu wa Mashariki mwa dunia zilipewa mazingatio katika utengenezaji wa filamu za Hollywood. La kusikitisha zaidi ni kuwa, ada na desturi hizo zinatambulishwa kwa jina la dini. Katika kipindi hicho filamu zinazotambulishwa kuwa za kungfu na sanaa ya Mashariki zilizusha makelele mengi mno. Hollywood na ulimwengu wa Magharibi kwa ujumla zilipigia debe filamu hizo na kuzizalisha kwa wingi.

Pamoja na hayo yote, kumekuwepo na baadhi ya filamu zinazowahimiza na kuwaelekeza watazamaji wake katika fikra na mitazamo ya kidini. Mfano wa filamu hizo ni kama ile ya Seven, Fight au Contact ambazo aghlabu zilizungumzia maudhui ya kupotea njia mwanadamu wa zama hizi na masuala kama vile adhabu na malipo ya hapa duniani na huko Akhera. Mfano bora zaidi wa filamu za aina hii ni ile ya "What Dreams May Come" iliyotengenezwa na Vincent Ward ambayo kimsingi ilihesabiwa kuwa ni hatua kubwa katika utengenezaji wa filamu za kidini huko Magharibi. Kwani filamu hiyo ilizungumzia kwa undani suala la malipo na adhabu ya Akhera kwa mtazamo wa kidini kupitia taswira na picha za kuvutia mno kuhusu ulimwengu wa Akhera kwa kutegemea maandiko ya vitabu vitakatifu. Filamu hiyo iliyotengenezwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ilifikisha ujumbe wa kidini na kiroho kwa kutumia picha na taswira. Aidha filamu za Krzysztof Kieslowski zinatambuliwa kuwa mfano mzuri wa mwelekeo wa watengeneza filamu wa sasa wa kuzungumzia masuala ya kiroho na kidini katika sanaa ya filamu. Filamu za msanii huyu wa Poland zinaelezea matakwa na irada ya Mwenyezi Mungu kuwa ndio inayoainisha kila kitu, na kwamba mwanadamu anapaswa kuelewa kwamba, kuwa mja wa Mwenyezi Mungu ndiyo daraja ya juu kabisa ya uhuru na pozo la roho yake.

Ukweli wa mambo ni kuwa, jamii ya sasa ya mwanadamu inamili na kuelekea kwenye masuala ya kidini ya kiroho. Mfano mdogo wa kuthibitisha ukweli huo ni jinsi Wamagharibi walivyoipokea filamu ya "Passion of The Christ" iliyotengenezwa na Mel Gibson, suala ambalo limeifanya filamu huyo kuchukua nafasi ya nane kati ya filamu zilizouzwa kwa wingi katika historia ya filamu duniani. Filamu ya Masaibu ya Masia "Passion of The Christ" ilitazamwa na idadi kubwa ya watu kwa sababu tu ya kuzungumzia maisha ya Nabii Isa Masih (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake) licha ya kuwa na vipengee vingi vya ukatili na utumiaji mabavu na pia opotoshaji wa baadhi ya masuala ya kihistoria. Katika makala ya wiki ijayo tutatupia jicho filamu za Mashariki na mwelekeo wa kutengeneza filamu za kidini katika eneo hilo la dunia.

Tunakamilisha makala yetu hii kwa kipande cha dialogi ya filamu ya Karamu ya Mwisho iliyotengenezwa na Ingmar Bergmen Anasema: Iwapo mwanadamu atamwamini Mungu hatakuwa tena na tatizo lolote, na kama hatakuwa na imani kamwe hatakuwa na njia ya ufumbuzi wa matatizo yake".