Iran yatoa wito kwa Uswidi iwaadhibu wale waliyoivunjia heshima Qur'ani Tukufu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i100178-iran_yatoa_wito_kwa_uswidi_iwaadhibu_wale_waliyoivunjia_heshima_qur'ani_tukufu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameitaka Uswidi kuwaadhibu wale waliohusika katika kitendo kiovu cha kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu katika nchi hiyo ya Skandinavia, huku akiionya kuhusu "maamuzi madhubuti" ya nchi za Kiislamu iwapo jambo hilo halitashughulikiwa.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Jul 22, 2023 00:56 UTC
  • Iran yatoa wito kwa Uswidi iwaadhibu wale waliyoivunjia heshima Qur'ani Tukufu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameitaka Uswidi kuwaadhibu wale waliohusika katika kitendo kiovu cha kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu katika nchi hiyo ya Skandinavia, huku akiionya kuhusu "maamuzi madhubuti" ya nchi za Kiislamu iwapo jambo hilo halitashughulikiwa.

Hossein Amir-Abdollahian alitoa wito huo katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Uswidi Tobias Billström siku ya Ijumaa, siku moja baada ya mtu mwenye chuki dhidi ya Uislamu kuivunjia heshima tena Qur’ani Tukufu nje ubalozi wa Iraq mjini Stockholm.

Wakati wa mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uswidi alisema serikali ya Uswidi inalaani kitendo hicho. Alisema polisi wa Uswidi wanaruhusu mikusanyiko pekee na mtu aliyeivunjia heshima Qur'ani Tukufu alitumia vibaya kibali cha mkusanyiko.

Waziri wa Iran amesema, “Mbali na kauli ya kulaani,  serikali ya Uswidi inapaswa kumkamata na kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria mtu aliyetenda kitendo hicho kisichosameheka.” Amir-Abdollahian ameonya kuwa iwapo Uswidi haitachukua hatua hiyo basi inapaswa kusubiri maamuzi madhubuti ya nchi za Kiislamu."

Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesikitika kwamba polisi wa Uswidi waliruhusu watu kutumia vibaya uhuru wa kujieleza ili kutusi maadili ya msingi ya Kiislamu, na kusema  yanayojiri Uswidi ni unyanyasaji wa wazi dhidi ya Waislamu.

Hali kadhalika ammesema, “Inapaswa kulaani vikali  vitendo vyote vya kuivunjia heshima Qur’ani na vitabu vingine vitakatifu na matakatifu mahali popote, mtu yeyote na kwa hali yoyote."  Waziri wa Mambo ya Njewa Iran amebaini kuwa, “Kuruhusu kurudiwa kwa hatua hizo kwa jina la uhuru wa kusema hakukubaliki .”

Qur'ani Tukufu

Amir-Abdollahian ameendelea kuhoji, “Je, Sweden, ambayo inadai kuwa mstari wa mbele katika haki za binadamu, inawezaje kuunga mkono kuvunjiwa heshima Qur’ani bila kujali chini ya siku 10 tangu kupitishwa azimio la Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa linalokashifu matusi ya kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini?” Alikuwa akiashiria azimio la chombo cha Umoja wa Mataifa la Julai 12 lililotaka mataifa kupitia upya sheria zao na kuziba mapengo yanayoweza kuruhusu kuenezwa chuki za kidini.

Azimio hilo lilikuja baada ya mhajiri huyo wa Kiiraki aliyeko Uswidi kuwasha moto kurasa kadhaa za Qur'ani Tukufu chini ya ulinzi wa polisi mbele ya msikiti mkubwa kabisa wa Stockholm mwishoni mwa mwezi wa Juni wakati wa siku kuu ya Idul Adha.

Uswidi imeruhusu mara kwa mara uchomaji wa Qur'ani Tukufu katika miaka ya hivi karibuni. Mwezi Januari, mwanasiasa mwenye msimamo mkali kutoka Sweden na Denmark alichoma nakala ya Qur'ani karibu na ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm.