Ghalibaf: Kuvunjiwa heshima itikadi za Waislamu duniani hakuwezi kuachwa hivi hivi
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ameilaani vikali serikali ya Sweden kwa kuandaa mazingira ya kuvunjiwa heshima tena Qur'ani Tukufu mjini Stockholm na kusema kuwa, kuzivunjia heshima itikadi za Waislamu duniani kuna gharama zake na serikali ya Sweden ndiyo inayobeba lawama.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Mohammad Bagher Ghalibaf amesema hayo leo Jumamosi wakati wa ufunguzi wa kikao cha wazi cha Bunge na kuongeza kuwa, serikali ya Sweden si mkweli katika madai yake kuwa inapinga kuvunjiwa heshima matukufu ya Qur'ani kwani haijachukua hatua yoyote ya maana ya kuzuia kutokea tena vitendo kama hivyo.
Amesisitiza kuwa, kuzijeruhi hisia za Waislamu duniani na kuvunjia heshima matukufu yao si jambo linaloweza kuachwa lipite vivi hivi bila ya kuchukuliwa hatua kali dhidi ya wahusika wote.
Spika wa Bunge la Iran ameongeza kuwa, kujitokeza kwa maelfu wananchi Waislamu wa Iran katika maandamano ya nchi nzima ya jana Ijumaa ya kulaani jinai hizo zinazofanywa na nchi za Magharibi dhidi ya matukufu ya Uislamu ilikuwa ni harakati muhimu sana iliyofanyika kwa wakati mwafaka na inatarajiwa kuwa serikali za nchi za Waislamu kote ulimwenguni nazo zitaungana na Waislamu wengine kuonesha ghera ya kidini na kupambana vilivyo na ushetani huu wa kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu.
Tukumbuke pia kuwa jana Ijumaa, Imamu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya hapa Tehran, Hujjatul Islam Sayyid Ahmad Khatami aliilaani serikali ya Sweden kwa kuruhusu kuvunjiwa heshima tena Qur'ani Tukufu na kuwataka Waislamu duniani kuchukua hatua kali za kuifanya nchi hiyo ya Ulaya Magharibi ijute kwa jinai yake hiyo.
Aidha khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya Tehran ameipongeza serikali na wananchi wa Iraq kwa hatua walizochukua zilizomlazimisha balozi wa Sweden kukimbilia kwenye ubalozi wa Marekani mjini Baghdad na kusisitiza kuwa, maadui wote wanapaswa kuelewa kwamba anayeichezea Qur'ani Tukufu anachezea mkia wa simba na ni wajibu kwa Waislamu kutoa majibu makali ya kuwafanya wajute, wale wote wanaochezea matukufu yao.