Iran na Iraq zalaani vikali kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Denmark
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i100194-iran_na_iraq_zalaani_vikali_kuvunjiwa_heshima_qur'ani_tukufu_nchini_denmark
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Denmark.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 22, 2023 07:19 UTC
  • Iran na Iraq zalaani vikali kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Denmark

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Denmark.

Baada ya raia mmoja wa Sweden mwenye asili ya Iraq kuivunjia heshima tena Qur'ani Tukufu mbele ya ubalozi wa Iraq mjini Stockholm juzi Alkhamisi, genge jingine lenye misimamo mikali ya kulia limemuunga mkono mtenda jinai huyo kwa kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu mbele ya ubalozi wa Iraq mjini Copenhagen, Denmark.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan'ani akilaani vikali kitendo cha genge hilo la nchini Denmark na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inamini kuwa serikali ya Denmark inahusika na kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini humo na inawataka viongozi wa nchi hiyo ya Ulaya kuwachukulia hatua watenda jinai hao kwani hilo kwa uchache ndilo wanalotarajia kuliona Waislamu zaidi ya bilioni mbili duniani kutoka kwa viongozi wa Copenhagen.

Waislamu wa Iran katika maandamano ya jana Ijumaa ya kulaani kuvunjiwa heshima tena Qur'ani Tukufu nchini Sweden

 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran vile vile ametoa mwito tena wa kuweko umoja na mshikamano wa serikali na mataifa yote ya Waislamu na wafuasi wa dini nyinginezo katika kukabiliana na magenge yanayopiga vita matukufu ya kidini na kuongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kufanya mazungumzo na nchi za Waislamu kuona hatua gani madhubuti zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya wanaovunjia heshima matukufu ya Kiislamu.

Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq nayo imelaani vikali kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Denmark na kuitaka jamii ya kimataifa kusimama kidete kukabiliana na utovu wa adabu huo.

Hayo yamekuja baada ya serikali ya Iraq kumtimua balozi wa Sweden nchini humo na baada ya Waislamu wenye hasira kuchoma moto ubalozi wa Sweden mjini Baghdad na kumlazimisha balozi wa nchi hiyo kwenda kujificha kwenye ubalozi wa Marekani mjini Baghdad.