Abdollahian: Nchi za Kiislamu zichukue msimamo imara dhidi ya kuvunjiwa heshima Qur'ani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu huko Sweden na Denmark, akisisitiza umuhimu wa kuchukuliwa msimamo thabiti wa nchi za Kiislamu katika kulaani na kuzuia vitendo hivyo.
Hossein Amir Abdollahian ameyasema hayo katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Kuwait, Salem Abdullah Al-Jaber Al-Sabah. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amepongeza misimamo ya serikali ya Kuwait katika kulaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Sweden na Denmark, na kutoa wito wa kufanyika kikao cha dharura cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na kutuma ujumbe mzito wa kulaani dharau na hujuma dhidi ya matukufu ya Kiislamu.

Amir Abdollahian pia ameashiria uhusiano mzuri uliopo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Kuwait na kusema: Tunaamini kuwa, kwa ushirikiano wa nchi za eneo hili tunaweza kuwa na eneo lenye amani, utulivu na maendeleo bila ya kuwepo madola ajinabi.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa kuwait, Salem Abdullah Al-Jaber Al-Sabah, sambamba na kukaribisha pendekezo la Amir Abdollahian la kufanyika kikao cha dharura cha mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu amesema: "Serikali ya Kuwait inalaani vikali chuki yoyote dhidi ya Qur'ani Tukufu na matukufu ya Kiislamu."
Alkhamisi iliyopita, raia wa Sweden mwenye asili ya Iraq, Salwan Momika kwa mara nyingine tena aliivunjia heshima Qur'ani Tukufu chini ya ulinzi na himaya kamili wa polisi wa Sweden mjini Stockholm.
Kafiri huyo mara hii alikanyaga na kupiga mateke nakala ya Kitabu hicho kitukufu cha Waislamu nje Msikiti mkuu mjini Stockholm, karibu na ubaloi wa Iraq. Ikumbukwe kuwa, Juni 28 wakati wa sikukuu ya Idul Adh'ha, Momika (37) aliidhalilisha Qurani Tukufu kwa kuichana na kuchoma moto.