Aug 01, 2023 13:36 UTC
  • Viongozi wa Iran na Oman watilia mkazo kupanuliwa mashirikiano baina ya nchi mbili

Viongozi wa Iran na Oman wamesisitiza na kutilia mkazo nia ziliyonayo Tehran na Muscat ya kuinua kwa kiwango na upeo wa juu zaidi uhusiano wa nchi mbili na kupanua zaidi maelewano baina ya pande mbili.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Seyed Ebrahim Raisi na Sultan wa Oman, Haitham bin Tariq Al Saeed, wamefanya mazungumzo kwa njia ya simu mapema leo ili kufanyia mapitio hatua zilizopigwa hadi sasa katika utekelezaji wa hati za ushirikiano zilizotiwa saini wakati wa ziara za pande mbili walizofanya viongozi hao; na kutilia mkazo nia ya Tehran na Muscat ya kuinua kwa kiwango na upeo wa juu zaidi uhusiano wa nchi mbili na kupanua zaidi maelewano baina ya pande mbili.
 
Viongozi wa Iran na Oman wamezungumzia pia ushirikiano wa kikanda na kimataifa wa pande hizo mbili katika nyuga mbalimbali.
Rais Ebrahim Raisi wa Iran (kulia) na Sultan Haitham bin Tariq Al Saeed wa Oman

Uhusiano kati ya Iran na Oman katika miongo ya karibuni siku zote umesimama juu ya msingi wa kuheshimu maslahi ya pande mbili licha ya mivutano iliyozuka katika Ghuba ya Uajemi na njama za Marekani za kushadidisha hisia za hofu na chuki dhidi ya Iran.

 
Viongozi wa Oman wanaamini kwamba, kuwa na uhusiano wa karibu na Iran kunatokana na kuzingatia uhalisia wa mambo na wanaichukulia Iran kama jirani mkubwa.
 
Nchi hizi mbili hazina mizozo yoyote ya ardhi wala ya mipaka baina yao.
 
Uungaji mkono wa Iran kwa Oman umekuwa wa sura chanya na wa kudumu katika kumbukumbu za kihistoria za Oman.../

 

Tags