"Serikali za Kiislamu ziyawekee vikwazo mataifa yanayoidhalilisha Qur'ani"
Mkuu wa Kamati ya Haki za Binadamu katika Majlsi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) ametoa mwito kwa madola ya Kiislamu kuziwekea vikwazo nchi zinazounga mkono vitendo vya kuvunjia heshima Kitabu Kitakafu cha Qur'ani.
Zohreh Elahian amenukuliwa akisema hayo na shirika la habari la Iran Press na kuongeza kuwa, mataifa ya Kiislamu yanapaswa kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo hivyo vya kuidhalilisha Qur'ani Tukufu.
Mbunge huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, "Huku nchi za Magharibi zikishirikiana katika mkondo wa chuki dhidi ya Uislamu, kuna haja kwa nchi za Kiislamu kuungana na kuziwekea vikwazo nchi ambazo zimefanya kuwa ajenda vitendo vya kuchoma moto Qur'an, na kuacha kuziuzia mafuta na nishati."
Bi Elahian aidha amebainisha kuwa, nchi za Kiislamu zinapaswa kususia bidhaa zinazozalishwa na nchi hizo, kama moja ya hatua za kukabiliana na jinai hiyo ambayo Wamagharibi wameihalalisha kwa kisingizio cha uhuru wa maoni.
Viongozi wa Iran ya Kiislamu wamekuwa wakisisitiza kuwa, uhuru wa maoni na kujieleza haipasi kuonekana kama idhini ya kitendo hicho cha fedheha cha kuvunjia heshima matukufu ya dini nyingine.
Vitendo viovu vya kuvunjia heshima kitabu kitukufu cha Qur'ani vimeendelea kulaaniwa na Waislamu na jamii ya kimataifa, akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ambaye ametangaza mshikamano wake na jamii ya Waislamu na kulaani hatua yoyote ya hujuma na propaganda chafu dhidi ya Uislamu na inayochochea mivutano.