Raisi: Waandishi wa habari ni daraja kati ya wananchi na viongozi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i100838-raisi_waandishi_wa_habari_ni_daraja_kati_ya_wananchi_na_viongozi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema waandishi wa habari ni daraja kati ya wananchi na wasimamizi wao na kuongeza kuwa: Waandishi wa habari wanaowakilisha vyombo vya habari, wanapaswa kujenga matumaini katika nyoyo za watu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 08, 2023 11:47 UTC
  • Raisi: Waandishi wa habari ni daraja kati ya wananchi na viongozi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema waandishi wa habari ni daraja kati ya wananchi na wasimamizi wao na kuongeza kuwa: Waandishi wa habari wanaowakilisha vyombo vya habari, wanapaswa kujenga matumaini katika nyoyo za watu.

Sayyid Ebrahim Raisi, ametoa pongezi kwa mnasaba wa Siku ya Mwandishi wa Habari na kuashiria umuhimu wa kazi ya waandishi habari. Ameongeza kuwa: Kalamu na waandishi wa habari, wapiga picha na wanahistoria wana nafasi ya juu, na wanapaswa kutumia zana na vifaa walivyonavyo kwa ajili ya kufikisha habari na taarifa kwa wakusudiwa.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaja nguvu kazi ya binadamu kuwa ni miongoni mwa mihimili muhimu zaidi katika uga wa kupasha habari na kusema: Licha ya kwamba, kutokana na maendeleo ya teknolojia, njia za kutoa habari zimeongezeka sana, lakini nguvu ya binadamu ndiyo inayopaswa kuwa na nafasi kuu na ipashe habari kwa watu kwa kutumia kalamu na sanaa yake kwa njia bora zaidi.

Rais Ebrahim Raisi amewapongeza waandishi habari na kusema: Mrengo wa vyombo vya habari vya adui unafanya kazi kupindua haki ionekana kuwa ni batili, na batili itambuliwe kuwa ni haki, na unataka kuchafua anga; Katika vita hivi vya utambuzi, kuna ulazima wa kutumia zana za ulinzi wa utambuzi kukabiliana na maadui. 

Rais Ebrahim Raisi

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, leo, Jumanne,  Agosti 8, 2023, inasadifiana na Siku ya Kumuenzi Mwandishi wa Habari hapa nchini Iran.

Miaka 25 iliyopita katika siku hii (Agosti mwaka 1998), wanamgambo wa kundi la Taliban waliwaua shahidi wanadiplomasia wanane wa ubalozi mdogo wa Iran pamoja na Mahmoud Sarmi, ripota wa Shirika la Habari la Jamhuri ya Kiislamu (IRNA) katika mji wa Mazar-e-Sharif, Afghanistan.

Kwa mnasaba huo, siku hii imepewa jina la Siku ya Mwandishi wa Habari katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.