Iran yazalisha bidhaa ya pili ya kimkakati katika sekta ya nyuklia
Maji mazito ni bidhaa ya pili ya kimkakati ya sekta ya nishati ya nyuklia baada ya uranium duniani na Iran ni moja kati ya nchi tano zinazozalisha bidhaa hii kwa usafi wa hali ya juu kiasi kwamba, nchi nyingi zinatazamia kununua maji mazito ya Iran licha ya vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Chini ya makubaliano ya nyuklia ya 2015, Iran inaruhusiwa kutumia maji mazito katika kinu chake cha nyuklia cha Arak kilichorekebishwa, lakini ikizalisha maji mazito ziada na pia ikirutubisha urani zaidi ya mahitaji yake lazima iuze bidhaa hizo katika soko la kimataifa.
Makubaliano hayo yanasisitiza kwamba, maji mazito yanayozalishwa Iran yasizidi tani 130, lakini kujiondoa kwa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mnamo Mei 2018 kumeiruhusu Iran kuongeza uzalishaji na kuwa na akiba ya bidhaa hizo mbili.
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, Mohammad Eslami, amewaambia waandishi wa habari wakati wa ziara yake ya hivi karibuni kwenye Kiwanda cha Uzalishaji wa Maji Mazito huko Khondab karibu na Arak kwamba maji mazito ya Iran yana wateja wengi. Asema Iran kwa sasa inawekeza kwenye maji mazito.
Eslami aliongeza kuwa, "wateja wetu wamegundua ubora wa juu na usafi wa maji mazito ya Iran."
Marekani ilikuwa imejitolea kununua tani 32 za maji mazito ya Iran kwa ajili ya matumizi ya vinu vyake vya nyuklia, lakini ilisitisha ununuzi huo baada ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump, kuachana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kutangaza vikwazo dhidi ya Iran.
Baada ya miaka mingi ya jitihada, tasnia ya nyuklia ya Iran sasa imeimarika kwa kiwango cha juu. Iran imestahamili ukaguzi mkubwa zaidi wa kimataifa uliowahi kutokea ulimwenguni ambao uliweka breki kwenye kasi ya maendeleo yake ya nyuklia, lakini pamoja na vizingiti hivyo sekta ya nyuklia ya Iran imeendelea kupiga hatua.
Hivi sasa mafanikio ya kiuchumi ya sekta ya nyuklia yanaanza kudhihirika.
Kulingana na Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, tasnia ya nyuklia ni mojawapo ya tasnia zenye thamani ya juu zaidi duniani.