Ebrahim Raisi: BRICS ina umuhimu mkubwa katika uchumi na biashara duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i101488-ebrahim_raisi_brics_ina_umuhimu_mkubwa_katika_uchumi_na_biashara_duniani
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, muungano wa kimataifa wa BRICS una nafasi na machango muhimu katika ushirikiano wa kiuchumi na kibiadhara duniani.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 25, 2023 23:28 UTC
  • Rais Ebrahim Raisi
    Rais Ebrahim Raisi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, muungano wa kimataifa wa BRICS una nafasi na machango muhimu katika ushirikiano wa kiuchumi na kibiadhara duniani.

Rais Ebrahim Raisi alisema hayo jana Ijumaa mara baada ya kurejea hapa Tehran akitokea Afrika Kusini alikohudhuria kikao cha 15 cha kilele cha kundi la BRICS kilichofanyika mjini Johannesburg. 

Rais Raisi ametoa ufafanuzi kuhusu matunda ya safari yake nchini Afrika Kusini kwa kusema kuwa, kundi la BRICS lina wanachama kuanzia kusini mwa Afrika hadi kaskazini mwa Afrika na kwenye bara la Asia hadi katika eneo la Amerika ya Latini tena nchi muhimu za maeneo hayo ndio wanachama wa BRICS.

Akiwa nchini Afrika Kusini, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alionana na viongozi mbalimbali wakiwemo wa nchi za Afrka kama Rais Macky Sall wa Senegal na Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni moja ya nchi sita zilizoalikwa kujiunga nakundi la BRICS

Katika mazungumzo yake na Rais Samia, Rais Ebrahim Raisi alisema kuwa Iran iko tayari kushirikiana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nyanja mbalimbali kama za kutoa huduma za uhandisi wa kiufundi, ujenzi wa mabwawa, mitambo ya kuzalisha umeme, kilimo na viwanda.

Rais Ebrahim Raisi alifanya mazungumzo hayo na Rais wa Tanzania pambizoni mwa mkutano wa kundi la Brics mjini Johannesburg Afrika Kusini na alikaribisha kwa mikono miwili kutanuliwa ushirikiano wa pande mbili na kusisitizia wajibu wa kuanzishwa tume ya pamoja ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kupanga mipango ya kuboresha kiwango cha mahusiano ya kiuchumi na kiutamaduni baina yao.