Iran: Tutaendeleza mpango wetu wa nyuklia na hatutoathiriwa na mashinikizo ya yeyote
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ira amesema: Tutaendelea mbele na mpango wetu wa amani wa nyuklia na kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kwa njia inayojenga na hatutoathiriwa na uingiliaji wa kisiasa, propaganda na mashinikizo ya madola ajinabi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Nasser Kan’ani, alisema hayo jana Ijumaa, tarehe 17 Septemba, wakati akijibu taarifa ya hivi karibuni ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na kusisitiza kwa mara nyingine tena kwamba, visiwa vitatu vya Bou Musa, Tonb Kubwa na Tonb Ndogo ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na ya milele ya ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwamba taarifa za mara kwa mara kama hizo za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi hazina itibari na thamani yoyote ya kisiasa na kisheria.
Ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara nia yake njema na kuishi kwa usalama na majirani zake kama ambavyo imekuwa ikitangaza mara zote kuwa visiwa hivyo vitatu ni sehemu ya ardhi ya Iran isiyoweza kutenganishwa na ardhi nyingine za nchi hiyo na hayo ni kwa mujibu wa misingi na sheria zinazokubalika za kimataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuzingatia mazungumzo yake ya pande mbili na serikali ya Kuwait, daima imekuwa ikitilia mkazo udharura wa kuweko ushirikiano wa kirafiki na wenye kujenga baina yake na majirani zake ikiwemo Kuwait. Amesema, bila ya shaka kujenga tabia ya kuzingatia maslahi ya pamoja kunaweza kutoa misingi inayofaa ya ushirikiano madhubuti wa kikanda.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, Jamhuri ya Kiislamu imeazimia kikwelikweli kuendeleza mpango wake wa amani wa nyuklia na kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kwa mujibu wa haki na wajibu ulio chini ya mpango huo.