Foreign Affairs: Ayatullah Khamenei ataifanya Iran dola kuu la Asia Magharibi
-
Ayatullah Ali Khamenei
Gazeti mashuhuri la Foreign Affairs la nchini Marekani limeandika kuwa Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ataifanya nchi hii kuwa dola kuu la Asia Magharibi.
Makala iliyochapishwa katika gazeti hilo imeeleza kwamba: Ayatullah Ali Khamenei ataigeuza Asia Magharibi kuwa eneo ambalo Iran itakuwa ndiyo dola lake kuu.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, Iran imefanikiwa vizuri kukabilina na kuvishinda vikwazo vya Magharibi.
Foreign Affairs imebainisha katika makala yake hiyo kwamba, viongozi wa Marekani mmoja baada ya mwingine walitumai kwamba mashinikizo ya kifedha na kidiplomasia dhidi ya Iran yangeilazimisha nchi hiyo kuachana na shughuli zake za nyuklia, lakini Wamagharibi walikosea katika mahesabu yao.
Gazeti hilo limeendelea kueleza kwamba ushirikiano wa Iran, Russia na China ni hatua inayolenga kuitenga Marekani katika ngazi ya kimataifa.
Makala hiyo ya gazeti la Foreign Affairs imeashiria ushirikiano kati ya Beijing, Moscow na Tehran na kubainisha kuwa, mwaka 2012 Iran na China zilitia saini makubaliano ya miaka 25 kwa ajili ya kushirikiana katika nyanja zote za kiuchumi.
Kwa mujibu wa Foreign Affairs, katika kipindi cha miezi kumi ya kwanza ya mwaka 2022, mauzo ya Russia kwa Iran yaliongezeka kwa asilimia 27 na nchi hizo mbili zilitia saini hati ya makubaliano ya uwekezaji wa Russia wenye thamani ya dola bilioni 40 katika miradi ya gesi ya Iran.
Gazeti hilo la Marekani limeongeza pia kuwa, kiwango cha ushirikiano wa Iran katika uga wa kimataifa kimeongezeka; na hilo linathibitishwa na uanachama wa hivi karibuni wa nchi hiyo katika jumuiya ya BRICS.../