Iran yakosoa uamuzi wa nchi 3 za Ulaya wa kuendeleza vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i102254-iran_yakosoa_uamuzi_wa_nchi_3_za_ulaya_wa_kuendeleza_vikwazo
Iran imelaani uamuzi wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani (E3) wa kuendeleza vikwazo vyao vya makombora ya balistiki na vinavyohusiana na nyuklia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kinyume na makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Tehran na madola sita makubwa ya dunia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 15, 2023 04:19 UTC
  • Iran yakosoa uamuzi wa nchi 3 za Ulaya wa kuendeleza vikwazo

Iran imelaani uamuzi wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani (E3) wa kuendeleza vikwazo vyao vya makombora ya balistiki na vinavyohusiana na nyuklia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kinyume na makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Tehran na madola sita makubwa ya dunia.

Vikwazo hivyo vilipaswa kumalizika mwezi ujao chini ya makubaliano hayo ambayo yanajulikana rasmi kwa jina la Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Nchi hizo tatu za Umoja wa Ulaya, almaarufu E3, ambazo ni sehemu ya mapatano hayo, hata hivyo, zilitangaza Alhamisi kwamba zinakusudia kuendeleza vikwazo hivyo zaidi ya muda uliowekwa.

Ikijibu uamuzi huo muda mfupi baadaye, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisema inauona kuwa "hatua isiyo halali," na kinyume na ahadi za nchi hizo tatu chini ya JCPOA na Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa -- ambalo liliidhinisha JCPOA.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeongeza kuwa,"Uamuzi huo ni sawa na hatua ya kujenga mvutano, ambayo inachukuliwa kwa nia mbaya."

Nchi hizo za Ulaya zilikuwa zimetaja sababu tatu za uamuzi wao huo, ikiwa ni pamoja na madai yao kwamba Iran imetuma ndege zisizo na rubani kwenda Russia, ambayo iko katika vita dhidi ya Ukraine, na kile wanachoita, uwezekano kwamba Tehran inaweza kuipatia Moscow makombora ya balestiki.

Jamhuri ya Kiislamu imekanusha madai yote mawili, na kusema inapinga vita.

Nchi hizo tatu za Ulaya pia zimeishutumu Iran kuwa imekiuka mapatano ya nyuklia ya JCPOA, zikirejelea hatua kadhaa za kisheria za nyuklia ambazo Jamhuri ya Kiislamu ilianza kuchukua baada ya Marekani kuondoka kinyume cha sheria katika mapatano ya JCPOA mwaka 2018 ambapo nchi hizo tatu zilishindwa kutoa fidia yoyote hasa kwa hasara iliyopatikana baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekumbusha kuwa, Iran ilianza hatua za kukabiliana na hatua  hiyo ya Marekani kwa kuzingatia vifungu vya 26 na 36 vya JCPOA vinavyowaruhusu washiriki wa mapatano hayo kupunguza ahadi zao iwapo pande nyingine zitafanya hivyo.

Aidha imebainisha kuwa Iran ilianzisha hatua za kulipiza kisasi baada ya kuzipa Washington na E3 mwaka mmoja ili kufidia ukiukaji wao wa JCPOA.

Taarifa hiyo, imeutaja  uamuzi wa nchi hizo tatu kuwa "usio na mantiki ya kisheria."

Wizara hiyo nayo imetahadharisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu itajibu uamuzi huo "haramu na wa uchochezi" kwa njia inayofaa na kwa kuzingatia haki zake chini ya JCPOA.