Qatar: Kutumwa pesa za Iran zilizoshikiliwa Korea Kusini kutamalizika wiki ijayo
Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed Bin Abdulrahman al-Thani, amesema kuwa mchakato wa kutuma fedha za Iran zilizokuwa zinashikiliwa nchini Korea Kusini kwenye akaunti za benki nchini Qatar kutamalizika wiki ijayo.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Iran IRNA, Al-Thani aliyasema hayo katika mazungumzo ya simu siku ya Alhamisi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian,
Qatar imekuwa mpatanishi katika mazungumzo yaliyopelekea makubaliano ya kubadilishana wafungwa kati ya Iran na Marekani ambayo yalitangazwa rasmi tarehe 10 Agosti.
Makubaliano hayo yanahusisha kuachiliwa kwa wafungwa watano kutoka kila upande pamoja na kuachiliwa dola bilioni 6 za Iran ambazo zilikuwa zinashikiliwa tangu 2018 katika benki mbili nchini Korea Kusini kwa sababu ya vikwazo vya Marekani.
Mchakato wa kuhamisha fedha hizo ulichukua zaidi ya mwezi mmoja hasa kwa sababu kulikuwa na kiwango maalumu cha fedha hizo za Iran ambazo zingeweza kuhamishwa kila siku kutoka benki za Korea Kusini.
Wakati wa mazungumzo yake ya simu na Al-Thani siku ya Alhamisi, Amir-Abdollahian aliipongeza Qatar kwa juhudi zilizopelekea kuachiliwa kwa wafungwa wa Iran nchini Marekani na kuachiliwa kwa fedha nchini Korea Kusini.
Wanadiplomasia hao wamesisitiza katika mazungumzo yao ya simu kwamba pande zote mbili za mpango wa kubadilishana wafungwa ziko tayari kubadilishana wafungwa siku iliyokubaliwa katika makubaliano yaliyopatanishwa na Qatar.
Iran tayari imewaachilia huru kutoka jela wafungwa watano wa Marekani waliokuwa chini ya mkataba huo na sasa wako katika kifungo cha nyumbani huku ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa pia ukifichua majina ya Wairani watano waliopangwa kuachiliwa kutoka jela za Marekani.