Iran: Tutajibu mapigo ya vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itajibu mapigo kwa hatua ya kujikariri ya Umoja wa Ulaya na Uingereza ya kuendelea kulisakama taifa hili kwa vikwazo.
Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika kikao na waandishi wa habari hapa Tehran na kueleza kuwa, hatua ya Ulaya ya kutofungamana na jukumu lake baada ya Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani kuiondoa nchi hiyo katika makubaliano ya JCPO, ni kucheza na wakati.
Amir-Abdollahian amebainisha kuwa, "Hatutakosa kujibu hatua za pande zingine; haiwezekani wanaitisha mazungumzo kwa upande mmoja, na kisha kwa upande wa pili wanazidisha mashinikizo dhidi ya Iran kwa kukariri sera ghalati."
Siku ya Ijumaa, serikali ya Uingereza ilitangaza kuyaongeza majina ya maafisa wa Iran kwenye orodha yake ya vikwazo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anasisitiza kuwa, "Sera hiyo ya uhasama na vikwazo itakabiliwa na jibu mwafaka la kulipiza kisasi la Iran."
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza kuwa: Kwa masikitiko, nchi tatu za Ulaya zinajaribu kukwepa majukumu yao kwa kuibana Iran kwa mashinikizo bandia.
Wakati huo huo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani hatua hizo zisizo za kisheria wala diplomasia za Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na kueleza kuwa, wanasiasa wa Ulaya wanapaswa kukiri kuwa, kuendelea na mienendo hiyo isiyo na maana si kwa maslahi yao.
Nasser Kan'ani amesema hayo baada ya Marekani na nchi kadhaa za Ulaya kutangaza vikwazo dhidi ya maafisa na wahariri wakurugenzi wa vyombo vya Jamhuri ya Kiislamu, mbali na kutoa matamshi ya uingiliaji dhidi ya taifa hili.
Marekani inajulikana kama nchi inayoongoza duniani kwa uwekaji vikwazo, ikiwa na rekodi ndefu zaidi ya kuziwekea nchi zingine kila aina ya vikwazo kwa ajili ya kufanikisha malengo na maslahi yake.