Iran yasema Marekani, E3 zilitumia vibaya IAEA kufikia malengo yao ya kisiasa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i102326-iran_yasema_marekani_e3_zilitumia_vibaya_iaea_kufikia_malengo_yao_ya_kisiasa
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema Marekani na nchi tatu za Ulaya katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 zilitumia vibaya Wakala wa Umoja wa Mataifa wa Nishati ya Atomiki kwa madumini ya kufikia malengo yao ya kisiasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 17, 2023 04:25 UTC
  • Iran yasema Marekani, E3 zilitumia vibaya IAEA kufikia malengo yao ya kisiasa

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema Marekani na nchi tatu za Ulaya katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 zilitumia vibaya Wakala wa Umoja wa Mataifa wa Nishati ya Atomiki kwa madumini ya kufikia malengo yao ya kisiasa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kan'ani alitoa kauli hiyo Jumamosi akijibu madai ya hivi punde yaliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) Rafael Grossi mapema jana dhidi ya Iran.

Katika taarifa yake, Grossi amelaani kile alichokiita hatua ya Iran "isiyo na uwiano na isiyo na kifani" ya kuondoa vibali vya  wakaguzi "wenye uzoefu zaidi" wa wakala waliopewa jukumu la kufanya shughuli za ukaguzi nchini Iran kwa mujibu wa Mkataba wa NPT.

Amedai hatua ya upande mmoja ya Iran inaathiri shughuli za ukaguzi za IAEA nchini Iran na "inapingana waziwazi na ushirikiano unaopaswa kuwepo kati ya Wakala huo na Iran."

Akijibu kauli hiyo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Kwa bahati mbaya, licha ya maingiliano mazuri, ya kujenga na ya kuendelea ya Iran na IAEA, nchi tatu za Ulaya na Marekani ziliitumia vibaya Bodi ya Magavana ya Shirika hilo kwa malengo yao ya kisiasa ... kwa lengo la kuharibu mazingira ya ushirikiano kati ya Iran na Shirika hilo. " Nchi tatu za Ulaya alizokusudia hapo ni Ufaransa, Uingereza na Ujerumani.

Kan'ani amesema Iran hapo awali ilionya dhidi ya matokeo ya juhudi hizo za kuingiza siasa katika kazi za kitaalamu za IAEA.

Msemaji huyo amesisitiza kuwa, Iran imefanya uamuzi huo kwa mujibu wa kifungu cha 9 cha makubaliano kati ya Jamhuri ya Kiislamu na IAEA.

Kan'ani kwa mara nyingine tena amezitaka nchi za Magharibi kuacha kutumia vibaya mashirika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na IAEA, na kuruhusu vyombo hivyo vya kimataifa kufanya shughuli zao za "kitaalamu na zisizoegemea upande wowote" bila mashinikizo ya kisiasa.

Amesema Iran inasisitiza ulazima wa kutoegemea upande wowote IAEA na itaendeleza ushirikiano wake chanya kwa kuzingatia makubaliano ya pande mbili.

Siku ya Jumatano, Bodi ya Magavana ya IAEA ilitoa taarifa iliyochochewa na nchi za Magharibi ambayo ilishutumu Iran kuwa haitekelezi ahadi zake katika masuala ya nyuklia.

Waraka huo uliotiwa saini na nchi 62 wanachama wa wakala huo, ulitoa wito kwa Iran kuchukua hatua za kushughulikia masuala ambayo bado hayajakamilika ya ulinzi na kuipa IAEA taarifa kuhusu vituo vyake vipya vya nyuklia.

Kan'ani ameikosoa  taarifa hiyo yenye msukumo wa kisiasa, akisema Iran na IAEA zimepata "maendeleo makubwa" katika kuimarisha ushirikiano kulingana na taarifa ya pamoja iliyotolewa mwezi Machi.