Sep 19, 2023 13:17 UTC
  • UNESCO yaziweka 'Caravanserai' za kihistoria za Iran kwenye orodha yake ya turathi za dunia

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeongeza Caravanserai' 54 za kihistoria za Iran katika orodha yake ya maeneo ya turathi za dunia.

Uamuzi huo ulitolewa katika kikao cha 45 cha Kamati ya Turathi za Dunia wa UNESCO katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh siku ya Jumapili, baada ya kuchunguza kwa makini Caravanserai  za Iran zinazopatikana katika mikoa 24 kote nchini.

Caravanserai kimsingi ni migahawa iliyokuwepo aghalabu katika kipindi cha “Barabara ya Hariri”. Barabara ya Hariri ni mjumuiko wa njia mbalimbali zilizokuwepo kipindi cha falme za kale zilizounganisha Afrika, Asia Magharibi, Arabia, Anatolia (Uturuki ya leo), Asia ya Kati na kuendelea mpaka China. Neno “Caravanserai” limetokana maneno mawili ya Kifarsi, yaani carvan (lenye maana ya msafara) na serai, linalomaanisha eneo lenye majengo yaliyoshikana.

Caravanserai hizo 54 za kihistoria zilichaguliwa miongoni mwa mamia baada ya kuidhinishwa na wajumbe wa kamati hiyo. Kwa msingi huyo Caravanserai ni turathi ya 27 ya utamaduni ya Iran iliyosajiliwa rasmi na UNESCO kama urithi wa dunia.

Kamati ya UNESCO imesema kwenye tovuti yake kwamba: "Caravanserai zilikuwa nyumba za wageni za kando ya barabara, zinazotoa makazi, chakula na maji kwa misafara, mahujaji na wasafiri wengine."

Picha ya  caravanserai nchini Iran

Kamati hiyo iliongeza kuwa: "Njia na maeneo ya misafara iliamuliwa na uwepo wa maji, hali ya kijiografia na wasiwasi wa usalama."

Misafara iliyoorodheshwa "inatambuliwa kuwa mifano yenye ushawishi na thamani zaidi ya misafara ya Iran, inayodhihirisha anuwai ya mitindo ya usanifu majengo, kukabiliana na hali ya hewa, na vifaa vya ujenzi, vilivyoenea katika maelfu ya kilomita na kujengwa kwa karne nyingi. Kwa pamoja, wanaonyesha mageuzi na mtandao wa misafara nchini Iran, katika hatua tofauti za kihistoria."

Mbali na kujumuishwa kwa caravanserai, kikao hicho pia kilipitia na baadaye kuliorodhesha Eneo Lililohifadhiwa la Dizmar, misitu ya milima ya Hyrcanian iliyoko kaskazini-magharibi mwa Iran, kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia wa UNESCO.

Iran pia imependekeza eneo la mandhari ya kitamaduni la Masuleh lisajiliwe katika Orodha ya Dunia ya UNESCO.

Tags