Raisi: Ikiwa Wamarekani watatimiza wajibu wao, tutafikia makubaliano mazuri
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i102498-raisi_ikiwa_wamarekani_watatimiza_wajibu_wao_tutafikia_makubaliano_mazuri
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: Marekani na nchi za Ulaya zinapaswa kutimiza makubaliano.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 21, 2023 04:18 UTC
  • Sayyid Ebrahim Raisi
    Sayyid Ebrahim Raisi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: Marekani na nchi za Ulaya zinapaswa kutimiza makubaliano.

Mwishoni mwa safari yake mjini New York, Rais wa Iran, Ebrahim Raisi alisema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba: Jamhuri ya Kiislamu haikuwahi kutoka kwenye meza ya mazungumzo, lakini baadhi ya nchi za Magharibi na Marekani ziliondoka kwenye meza ya mazungumzo kwa sababu ya mahesabu yao yasiyo sahihi na kwa kutegemea ghasia zilizotokea Iran; lakini baada ya muda, walipoona taifa la Iran limewafanya washindwe kufikia malengo yao, waliomba tena kurejea kwenye meza ya mazungumzo ya nyuklia.

Rais Ebrahim Raisi ameongeza kuwa: Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitapuuza haki za taifa la Iran kuhusiana na suala hilo na inasubiri hatua za kivitendo za pande nyingine katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Katika upande mwingine, Sayyid Ebrahim Raisi amesema kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haioni kikwazo chochote katika kuanzisha uhusiano na Misri, na kwamba suala hilo limetangazwa kwa upande wa Misri.

Kuhusu kadhia ya Palestina, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amebainisha kuwa, suala la uhuru wa Palestina daima limekuwa kadhia nambari moja ya Ulimwengu wa Kiislamu, hivyo basi kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel ni sawa na kuwasaliti na kuwadunga jambia mgongoni wananchi na wanamapambano wa Palestina. Amesema Juhudi za utawala wa Kizayuni za kutaka kuanzisha uhusiano na baadhi ya serikali za eneo Magharibi mwa Asia hazitawadhaminia usalama kwa vyovyote vile, kwa sababu mataifa ya eneo hilo yanauchukia sana utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na miaka 75 ya ukandamizaji unaofanywa na utawala huo dhidi ya taifa la Palestina.

Watoto wa Kipalestina waliouawa na jeshi la Israel

Vilevile amesisitiza kuwa: Mpango wa nyuklia wa Iran ni wa amani kabisa na waangalizi wa kimataifa wamethibitisha suala hili.

Kuhusu vita vya Ukraine, Raisi amesema kuwa: "Katika mazungumzo ya mwisho niliyofanya na Rais Vladimir Putin wa Russia, alisisitiza kwamba shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO ndilo linalotaka kuendeleza vita na halitaki vita hivi vifikie tamati.

Sayyid Ebrahim Raisi amerejea mapema leo mjini Tehran akitokea New York, Marekani alikoshiriki Mkutano wa 78 wa Umoja wa Mataifa.