Mhusika mkuu wa shambulio la kigaidi huko Shah Cheragh ahukumiwa kifo
Mhusika mkuu wa shambulio la kigaidi kwenye Haram Takatifu ya Hadhrat Ahmad bin Musa (AS) maarufu kama Shah Cheragh mjini Shiraz kusini mwa Iran, amehukumiwa kifo.
Hayo yamedokezwa na Jaji Mkuu wa Mkoa wa Fars Kazem Mousavi ambaye amesema Mshukiwa mkuu, Rahmatollah Nowruzof kutoka Tajikistan, alihukumiwa kifo mara mbili kwa kosa la "muharabah" (kupigana vita dhidi ya Mwenyezi Mungu), uasi wa silaha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, na kula njama dhidi ya usalama wa Iran. Shirika la habari la Mizan, linalofungamana na Idara ya Mahakama ya Iran limemnukuu, Jaji Mousavi akisema kwamba washtakiwa katika daraja la pili na la tatu walipewa vifungo vya miaka mitano jela kila mmoja, na waliepushwa na adhabu ya kifo kwa kosa 'muharabah' na ufisadi katika ardhi kwa kuwa "hawakujua nia mbaya" ya mhusika mkuu.
Ripoti hiyo inakuja kufuatia kusikilizwa kwa kesi tatu katika mahakama ya ndani ya mapinduzi katika mji wa Shiraz. Waliohukumiwa wamepewa siku 20 kukata rufaa dhidi ya hukumu hizo.
Mnamo Agosti 13, Nowruzof, mwenye lakabu ya Aslamyar, alifyatua risasi katika Haram ya Shah Cheragh, na kuua watu wawili na kujeruhi watu saba. Alikuwa amebeba bunduki na na risasi 240, ambapo alifyatua risasi 11 kabla ya kukamatwa.
Shambulio hilo lilitokea chini ya mwaka mmoja baada ya gaidi mwingine aliyekuwa na silaha kuvamia eneo hilo takatifu la ibada mnamo Oktoba 26, 2022, na kuwaua wafanyaziara 15, wakiwemo wanawake na watoto, na kujeruhi wengine kadhaa kabla ya kupigwa risasi na kujeruhiwa na vikosi vya usalama. Gaidi huyo alifariki baada ya kufyatuliwa risasi na walinzi. Aidha wahusika wengine wa kitendo hicho cha kigaidi walinyongwa mwezi Julai
Katika taarifa yake tarehe 18 Agosti, Wizara ya Usalama ya Iran ilisema imemkamata mshukiwa mwenye uhusiano na Daesh ambaye alitekeleza jukumu la "muhimu zaidi" katika shambulio baya la pili la kigaidi kwenye Haram ya Shah Cheragh.
Taarifa hiyo ilisema magaidi 196 wa kitakfiri walikamatwa au kuuawa kati ya mashambulio hayo mawili ya kigaidi kwenye Haram ya Shah Cherag na wote hawakuwa Wairani bali walikuwa ni raia Jamhuri ya Azerbaijan, Tajikistan na Afghanistan.