Amir Abdollahian: Mizani ya Iran ni mienendo ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i102616-amir_abdollahian_mizani_ya_iran_ni_mienendo_ya_marekani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: Kipimo cha Iran ni mienendo ya Marekani; na matendo na mienendo ya serikali ya Marekani ni ya kindumakuwili na msingi wake ni kucheza na wakati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 24, 2023 04:27 UTC
  • Hossein Amir Abdollahian
    Hossein Amir Abdollahian

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: Kipimo cha Iran ni mienendo ya Marekani; na matendo na mienendo ya serikali ya Marekani ni ya kindumakuwili na msingi wake ni kucheza na wakati.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir Abdollahian, ameyasema hayo katika mkutano wa wanafikra, mabalozi na wanadiplomasia wastaafu wa Marekani mjini New York.

Amir Abdollahian amesema: Siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kurejea kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA ikiwa ni mapatano ya kimataifa, lakini mielekeo ya serikali ya Marekani ni ya kindumakuwili na imejikita katika kucheza na wakati.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa: Iwapo serikali ya Marekani itakuwa na azma ya kweli, mazungumzo yanaweza kukamilika kwa muda mfupi na kisha pande zote zitarejea kwenye JCPOA na utekelezaji kamili wa majukumu yake.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameutaja mgogoro wa Afghanistan kuwa ni miongoni mwa migogoro iliyokita mizizi katika eneo hilo la Asia, ambayo imekuwa na taathira na madhara mengi katika kanda hiyo, ikiwa ni pamoja na hatari ya kuenea ugaidi na mgogoro wa wakimbizi na wahajiri.

Amir Abdollahian ameisisitiza haki ya wananchi wa Palestina ya kupambana dhidi ya uvamizi na kukaliwa kwa mabavu nchi yao, na ameutaja mpango wa kidemokrasia uliopendekezwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu utatuzi wa mgogoro wa Palestina kuwa ni suluhisho la kimantiki, kisheria na la kidemokrasia la kumaliza mgogoro huu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Jamhuri ya Kiislamu haitambui vita kuwa suluhu la mgogoro wowote, sio Ukraine, Afghanistan, Syria, Yemen wala Sudan, na kwamba mgogoro wa Ukraine na mivutano kati ya Russia na Ukraine lazima utatuliwe kwa njia ya siasa na mazungumzo.

Amir Abdollahian amekutaja kutuma silaha kwa upande mmoja wa vita hivyo kuwa kunachochea vita na wala sio mchango wa kurejesha amani, na akatangaza kuwa Iran itaendeleza juhudi za kusaidia usitishaji vita na kuzirejesha pande husika kwenye meza ya mazungumzo.