Sep 26, 2023 03:10 UTC
  • Iran yasema  ina haki ya kujibu tabia ya kiburi ya Israel

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ina haki ya kujibu tabia ya kiburi ya utawala wa Israel, siku chache baada ya waziri mkuu wa utawala huo ghasibu, Benjamin Netanyahu kusema Iran "lazima ikabiliwe na tishio la kihakika la nyuklia."

Akizungumza katika Kikao cha 67 cha Kawaida cha Baraza Kuu la Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) mjini Vienna siku ya Jumatatu, Mohammad Eslami, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) ameashiria matamshi ya Netanyahu katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusema, hakuna shaka kuwa kimya cha jamii ya kimataifa kimeutia moyo utawala wa Israel.

Amesema ni wazi kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina haki ya kujibu chockochoko za utawala wa Kizayuni.

Wakati wa hotuba yake katika kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa, Netanyahu alionya kuhusu kile alichokiita eti "laana ya Iran ya nyuklia" na kuishutumu Tehran kwa kutumia na "kuwapa mabilioni ya fedha washirika wake wa ugaidi."

Mtawala huyo katili wa Israel alisema, "Iran lazima ikabiliane na tishio la kiuhakika la nyuklia. Maadamu nitakuwa waziri mkuu wa Israel, nitafanya kila niwezalo kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia.”

Ujumbe wa kidiplomasia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa umepuuzilia mbali madai yasiyo na msingi ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Israel Benjamin Netanyahu na kusema ni "maonesho ya vichekesho" dhidi ya mpango wa amani wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na shughuli zake za kieneo.

Wakati huo huo, Eslami pia amesema vitisho vya Israel dhidi ya wanasayansi wa nyuklia wa Iran ni ukiukaji wa Mkataba wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni mwanzilishi wa mpango wa eneo lisilo na silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati, inabainisha wasiwasi wake kuhusu mpango wa siri wa kijeshi wa nyuklia wa utawala wa Israel.