Jeshi la Wanamaji la Iran kujenga kambi ya kudumu barani Antaktika
Mkuu wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Admeri Shahram Irani amedokeza kuwa jeshi hilo lina mpango wa kujenga kituo cha kudumu katika bara la Antaktika, ikiwa ni pamoja na kuanzisha kituo cha kudumu cha harakati za kijeshi na kisayansi.
Akizungumza na kanali ya televisheni ya IRIB TV1 wakati wa kipindi cha kuadhimisha kumbukumbu ya vita vya Iraq vya 1980-88 dhidi ya Iran, Admeri Irani amesema: "Mpango wetu wa baadaye ni kuinua kwa fahari bendera ya Iran huko Antaktika, na kufanya juhudi shirikishi za kijeshi na kisayansi katika eneo hilo."
Alipoulizwa kama hii inamaanisha kujenga kituo cha kudumu huko Antarctica, Admeri Iran alisema, "Inshallah (Mwenyezi Mungu akipenda)."
Akifafanua kuhusu nukta hiyo amesema, "Sio kazi ya kijeshi tu. Inabidi kuwe na kazi ya kisayansi na wanasayansi wetu wapenzi wanajiandaa kutekeleza juhudi za pamoja kwa mujibu wa miongozo” ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei.
Kamanda huyo alisema mpango huo kabambe wa siku zijazo unaashiria uwezo mkubwa uliopo ndani ya Jeshi la Wanamaji la Iran.
Ameongeza kuwa: "Mwaka jana, kwa kufuata miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, tulijaribu kuanzisha uwepo thabiti wa baharini (duniani kote). Hili lilifanyika pamoja na kuwepo changamoto mbalimbali njiani, muhimu zaidi ikiwa ni kwamba hatukuwa na uzoefu wa kazi kama hiyo hata kidogo.”
Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Iran aliendelea kuangazia jitihada zisizo na kikomo za baadhi ya nchi kuzuia uwepo wa Iran baharini, akisema: "Ndani ya Jeshi la Wanamaji, tulisambaratisha vikwazo tumeweza kufikia mafanikio makubwa ya kupeleka misafara 86 ya meli za kivita katika maji ya kimataifa licha ya njama za madola ajinabi."
Meli za 86 za wanamaji wa Iran, ambazo zilisafiri duniani kote kutoka mji wa bandari wa Bandar Abbas mnamo Septemba 20, 2022, zilirejea nyumbani Mei 20 baada ya kuzunguka dunia. Imevunja rekodi rasmi ya umbali ambao flotilla ya Irani imesafiri katika maji ya kimataifa.
Msafara wa 86 wa Meli za Kivita za Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliondoka katika Bandari ya Bandar Abbas kusini mwa Iran Septemba 2022 na ulirejea nchini Mei 20 baada ya safari ya kuzunguka dunia kama sehemu ya juhudi za Jamhuri ya Kiislamu za kupanua uwepo wake kijeshi katika bahari za mbali.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliitaja kazi hiyo yenye mafanikio na fahari iliyofanywa na Msafara 86 la Wanamaji wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuzunguka dunia nzima kuwa ni matokeo ya kazi ngumu, nia thabiti, kujiamini, uwezo wa kubuni, maarifa ya hali ya juu ya kijeshi, uongozi bora na "ujasiri na kusimama imara mkabala wa mashaka ya aina mbalimbali."