Sep 30, 2023 04:46 UTC
  • Rais wa Iran alaani mashambulizi pacha ya kigaidi Pakistan

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amelaani mashambulizi mawili ya kigaidi yaliuoua makumi ya watu katika jimbo la kusini magharibi la Balochistan nchini Pakistan.

Katika ujumbe wake wa pole kwa Rais Arif Alvi wa Pakistan, Rais wa Iran amesema 'Matendo pofu kwa mara nyingine yameonyesha namna magaidi ambao hawana ufahamu wowote kuhusu mafundisho ya rehema ya Uislamu, hawana malengo yoyote isipokuwa kuibua mifarakano miongoni mwa Waislamu."

Aidha Sayyid Raisi ametuma salamu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Pakistani hususan kwa wahanga hujuma hizo, na kuwaombea ahueni ya haraka majeruhi wa mashambulizi hayo ya kikatili ya jana. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ipo tayari kushirikiana na Pakistan katika vita dhidi ya aina zozote za ugaidi na misimamo mikali ya kufurutu ada.

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaka jamiii ya kimataiifa hasa mataifa ya Waislamu kutoa radiamali zao madhubuti dhidi ya vitendo hivyo vya kikatili, ili visijikariri.

Wakati huohuo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kana’ani sambamba na kulaani hujuma hizo amesema mashambulizi hayo ni "mfano wa wazi wa magaidi kujitenga na mafundisho ya rehema ya Mtume Muhammad (SAW)".

Mlipuko wa kwanza ulitokea karibu na msikiti katika mji wa Mastung eneo la Attahul Munim jana Ijumaa wakati waumini wa Kiislamu walipokuwa wamekusanyika kusherehekea Maulidi ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW), na kuua watu zaidi ya 55 na kujeruhi wengine zaidi ya 80.

Saa chache baada ya mlipuko huo katika jimbo la Balochistan, mlipuko mwingine ulikumba msikiti mmoja katika mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa ambao pia unapakana na Afghanistan, na kuua na kujeruhi watu kadhaa.

Tags