Amir-Abdollahian: Mauaji ya watoto wachanga ni sifa ya utawala wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i102984-amir_abdollahian_mauaji_ya_watoto_wachanga_ni_sifa_ya_utawala_wa_israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian, anasema utawala haramu wa Israel unajulikana kwa kuua watoto wa Kipalestina ambapo pia mwaka huu imeua idadi kubwa ya watu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 02, 2023 23:16 UTC
  • Amir-Abdollahian: Mauaji ya watoto wachanga ni sifa ya utawala wa Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian, anasema utawala haramu wa Israel unajulikana kwa kuua watoto wa Kipalestina ambapo pia mwaka huu imeua idadi kubwa ya watu.

Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika ujumbe wake ukurasa wa X kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mauaji ya mvulana Muhammad al-Durrah aliyekuwa na umri wa miaka 12 aliyepigwa risasi na askari wa Israel akiwa mikononi mwa babake katika Ukanda wa Gaza.

Akiomboleza kifo hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, "Kuuwa watoto wachanga ni sifa ya utawala haramu  wa Israel", na kubainisha kwamba "tangu mwanzoni mwa 2023, watoto 40 wa Kipalestina wameuawa shahidi na utawala wa kibaguzi wa Israel."

Muhammad al-Durrah aliuawa kwa silaha ya askari katili wa Israel mnamo Septemba 30, 2000, siku ya pili ya Intifadha (mwamko) dhidi ya utawala wa Israel.

Video iliyorekodi tukio hilo ilimuonyesha Muhammad na baba yake, Jamal, wakijikinga na pipa la zege la maji huku wakimiminiwa risasi na wanajeshi katili wa Israel, na baada ya  muda mfupi Muhammad aliuawa shahid, ukatili ambao ulizua hasira duniani kote.

Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, Israel imeongeza mashambulizi katika vijiji na miji ya Palestina katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu. Kutokana na mashambulizi hayo makumi ya Wapalestina wameuawa na wengine wengi kukamatwa.

Zaidi ya Wapalestina 200 wameuawa mwaka huu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Gaza. Idadi kubwa ya mauaji hayo yamerekodiwa katika Ukingo wa Magharibi.

Umoja wa Mataifa umesema, mwaka 2023 ndio mwaka mbaya zaidi kwa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi tangu uanze kufuatilia vifo karibu miongo miwili iliyopita.

Kulingana na UN, hapo awali, mwaka 2022 ulikuwa mwaka mbaya zaidi ambapo Wapalestina 150 waliuawa, kati yao 33 walikuwa watoto wadogo,

Kuongezeka kwa idadi ya vifo mwaka jana kulifanya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kulaani jinsi Wapalestina wanavyotendewa, ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya nyumba zao na uharibifu wa mali na milki zao.