Muirani aliyevumbua dawa dhidi ya saratani atunukiwa medali ya dhahabu ya dunia
Mvumbuzi Muirani aliyevumbua dawa ya kuzuia ugonjwa wa saratani (cancer) ametunukiwa medali ya dhahabu katika Mashindano ya Kimataifa ya Uvumbuzi na Ubunifu ya Uswisi ya mwaka 2023.
Shirika la habari la Farsi limeripoti kuwa, Sayyid Hamad Mortazavi mvumbuzi wa Kirani na mwanachama wa Shirikisho la Wavumbuzi Duniani ameshinda medali ya dhahabu ya Mashindano ya Kimataifa ya Shirikisho la Kimataifa la Wavumbuzi (IFIA) huko Geneva Uswisi kufuatia uvumbuzi aliofanya kwa jina la "Kidonge Endelevu cha Kuzuia Saratani na Matibabu kwa Seli Zilizoshambuliwa".
Katika duru ya mashindano hayo, wavumbuzi 1500 wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali duniani zikiwemo Canada, Marekani, Australia, Morocco, Indonesia, Uturuki, Iran, Russia, Qatar, Bahrain, Uingereza, China, Hong Kong, Malaysia, Thailand, Imarati na Poland walichuana na mwakilishi huyo wa Iran.
Mortazavi ameeleza kuwa, uvumbuzi aliofanya ni kwa ajili ya matibabu ya kuzia na kudhibiti ugonjwa wa saratani ambayo husaidia kuweka sawa mfumo wa kinga ya mwili na kupambana na saratani ipasavyo hadi hatua ya kwanza ambapo uvimbe wa ugonjwa huo huwa katika hali ya kuongezeka.
Ameongeza kuwa, dawa hiyo aliyoivumbua ina taathira kubwa katika kuzuia ugonjwa wa saratani. Dawa zinazotengenezwa hapa nchini zina ubora wa hali ya juu ambapo makampuni mbalimbali katika sekta hiyo yana uwezo mkubwa wa kuuza dawa hizo kwa nchi mbalimbali duniani.