Matamshi ya viongozi wa Iran katika Siku ya Kimataifa ya Quds
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa taifa la Iran litaendelea kuunga mkono vilivyo haki za wananchi madhlumu wa Palestina na kueleza kuwa Tehran kamwe haitawaacha peke yao wananchi na muqawama wa Palestina mbele ya utawala katili wa Kizayuni.
Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo katika maandamano ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds hapa Tehran na kuongeza kuwa wananchi wa Palestina wanapaswa kujua kuwa, kamwe hawako pekee yao na kwamba muqawama utapata ushindi kwa usaidizi na uungaji mkono wa nchi zinazopigania uhuru wa taifa hilo ikiwemo Iran.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, utawala wa Kizayuni ambao unatambuliwa kama kituo cha Marekani katika eneo hili hauheshimu sheria yoyote ya kimataifa wala misingi ya ubinadamu.
Naye Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds kuwa: Leo hii siasa za dhulma katika eneo la Mashariki ya Kati zimekuwa tatizo kubwa kwa eneo hili na kwa amani na usalama wa dunia nzima.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa makundi ya kitakfiri na waungaji wao mkono wao, mwaka huu na katika miaka ya nyuma yamekuwa yakiungwa mkono na utawala wa Kizayuni, na ndio maana yameekeleza mashambulizi yao dhidi ya Waislamu badala ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni. Wakati huo huo Is'haq Jahangiri Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesema kuwa, kushiriki kwa wingi na kwa hamasa kubwa kama kawaida yao wananchi wa Iran katika Siku ya Kimataifa ya Quds ni hatua muhimu sana na kwamba kuwaunga mkono na kuwatetea wananchi madhlumu wa Palestina ni moja ya malengo muhimu ya taifa la Iran katika kulipigania taifa madhlumu la Palestina.