Salami: Operesheni ya ardhini Gaza itawatafuna wanajeshi wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i103968-salami_operesheni_ya_ardhini_gaza_itawatafuna_wanajeshi_wa_israel
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amelionya vikali jeshi la Israel kwamba, operesheni ya nchi kavu dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza linalokaliwa kwa mabavu haitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kutafunwa na kuangamizwa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 26, 2023 08:54 UTC
  • Salami: Operesheni ya ardhini Gaza itawatafuna wanajeshi wa Israel

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amelionya vikali jeshi la Israel kwamba, operesheni ya nchi kavu dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza linalokaliwa kwa mabavu haitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kutafunwa na kuangamizwa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni.

Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la SEPAH ametoa indhari hiyo leo Alkhamisi akihutubu katika hafla ya jeshi la IRGC katika mji mtukufu wa Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran na kuongeza kuwa, Kushindwa (Wazayuni) katika Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ni moja ya vipigo vikubwa vya aina yake ambavyo havijawahi kushuhudiwa, na ambavyo vimeziyumbisha Marekani, Uingereza pamoja na Israel yenyewe.

Meja Jenerali Salami ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel, si tu kwamba umepata pigo kubwa bali pia umeshindwa kwa fedheha na wanamuqawama wa Palestina. Kuangamizwa Wazayuni zaidi ya 1,500 wakiwemo mamia ya wanajeshi ya utawala huo ghasibu, ni sehemu ndogo ya matunda ya Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ya wanamapambano wa Palestina iliyoanza Oktoba 7.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa: Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa imeyumbisha kisiasa na kiusalama mfumo wa kistratejia wa adui na kuongeza kwamba, utambulisho bandia wa utawala wa Kizayuni umeporomoka.

Hujuma za anga za Wazayuni Ukanda wa Gaza

Meja Jenerali Salami amesema Wazayuni katika ulimwengu wa Kiislamu ni kama saratani iliyopandikizwa katika eneo, ambayo kazi yake ni kumwaga damu kila mara. Ameyataka mataifa ya Kiislamu kuwa na umoja na mshikamano ili kuvunja njama na jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina.

Salami amesema viongozi wa Marekani na nchi za Ulaya wanapigana vikumbo kwenda Tel Aviv kujaribu kuupa maisha bandia utawala wa Kizayuni wa Israel ili utawala huo ambao uko katika ncha ya kutokomea uendelea kupumulia kwa mashine.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: Mwenyezi Mungu hufanya miujiza katika kila zama, na Gaza hivi sasa ndio mfano wa miujiza ya Nabii Musa AS, na iwapo Waisraeli watathubutu kuingia Gaza, zimwi la Gaza litawatafuna na watazikwa huko.