Amir-Abdollahian akutana na Guterres, asisitiza uungaji mkono wa Iran kwa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i104028-amir_abdollahian_akutana_na_guterres_asisitiza_uungaji_mkono_wa_iran_kwa_palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu kwa wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina mbele ya jinai za kinyama za utawala wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 28, 2023 03:41 UTC
  • Amir-Abdollahian akutana na Guterres, asisitiza uungaji mkono wa Iran kwa Palestina

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu kwa wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina mbele ya jinai za kinyama za utawala wa Israel.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo alipokutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres siku ya Ijumaa mjini New York Marekani ambako alifikia kuhudhuria mkutano usio wa kawaida wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu kadhia ya Palestina.

Amir-Abdollahian amemfahamisha bayana Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwamba: "Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono mapambano ya ukombozi ya watu wa Palestina na muqawama kwa lengo la utimilifu kamili wa haki zao za kibinadamu, na msimamo huo ni kati ya misingi ya sera za nje za Iran."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha amelaani vikali mauaji ya kimbari yanayoendelea kutekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Palestina la Ukanda wa Ghaza.

Amir-Abdollahian amemfahamisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwamba kimya cha baadhi ya nchi pamoja na uungaji mkono wa Marekani kumeupa kiburi utawala ghasibu wa Israel kuendeleza jinai dhidi ya raia wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan,

Watoto wa Ghaza wakiwa juu ya magofu ya nyumba zao ambazo zimeharibiwa katika hujuma ya kinyama ya utawala katili wa Israel

Aidha amesisitiza kuwa, Iran inaunga mkono suluhu ya kisiasa itakayowezesha kukomesha mara moja jinai zinazoendelea za utawala wa Israel dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari huko Ghaza, kupelekwa misaada ya kibinadamu Ghaza na kuzuia wakazi wa Ghaza kuyahama makazi yao kwa lazima."

Ameonya kuwa kuendelea jinai za kivita za utawala dhalimu wa Israsel dhidi ya Ghaza kutafungua mlango wa kupanuka vita vinavyoendelea na kuandaa medani mpya dhidi ya utawala wa Kizayuni katika eneo zima.

Amir-Abdollahian amesema amani endelevu itapatikana tu pale utawala wa Kizayuni wa Israel utakapoacha kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina, kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi yao, kuandaliwa kura ya maoni itakayowashirikisha wakaazi wote wa awali wa Palestina, na hatimaye kuundwa taifa huru la Palestina mji mkuu wake ukiwa mji mtakatifu wa Quds.

Kwa upande wake, Guterres ametilia mkazo nafasi ya kipekee ya Iran katika eneo na kuhimiza kuendelezwa juhudi za kidiplomasia za Jamhuri ya Kiislamu.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameelezea hali ya sasa ya kibinadamu huko Ghaza kuwa ni janga, na kuzitaka pande zote kuwezesha kusitishwa mara moja vita na kupelekwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo linalozingirwa na utawala wa Kizayuni.