Kan'ani: Jinai zinazofanywa na Wazayuni huko Ghaza ni mauaji ya kimbari
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amechapisha picha za watoto waliouawa shahidi na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ghaza na kuzitaja jinai zinazofanywa na Wazayuni katika eneo hilo kuwa ni mauaji ya wazi ya kimbari.
Katika kukabiliana na jinai za mara kwa mara za utawala wa Kizayuni, siku ya Jumamosi tarehe 7 Oktoba 2023 Wapiganaji wa muqawama wa Palestina walianzisha operesheni ya kipekee iliyopewa jina la Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya uhalifu na jinai za utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.
Tangu kuanza kwa operesheni hiyo, jeshi la utawala haramu wa Israel ambalo halina uwezo wa kupambana na wapiganaji wa muqawama, limekuwa likishambulia kwa mabomu maeneo ya makazi ya raia, hospitali, vituo vya kidini na shule za Ghaza, na matokeo yake, zaidi ya watu elfu 7 na 700 wameuawa shahidi na wengine karibu elfu 20 wamejeruhiwa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana (Jumapili) alichapisha picha za watoto waliouawa shahidi katika mashambulizi ya Wazayuni huko Ghaza kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuandika: Picha hizi ni mfano mdogo sana wa jinai za jeshi la wahalifu la utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.
Mauaji hayo ya Israel katika Ukanda wa Gaza yamelaaniwa na wanasiasa, jumuiya za kimataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Majuzi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisisitiza katika hotuba yake katika Baraza la Usalama kwamba mashambulizi ya hivi karibuni ya wapigania uhuru wa Palestina hayawezi kuhalalisha adhabu ya pamoja inayotolewa na Israel dhidi ya watu wa Gaza.
Katika sehemu ya hotuba yake, Guterres alisema: Ni muhimu kujua kwamba, mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 mwezi huu wa Oktoba dhidi ya jeshi na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina, hayakutokea bila sababu, na kwamba wananchi wa Palestina wamekuwa wakisulubiwa na uvamizi huo kwa zaidi ya miaka 50.