Iran yaitaka ICC kuharakisha kufuatilia jinai za Israel Ukanda wa Ghaza
Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ametaka kuharakishwa ufuatiliaji wa kisheria wa hali ya Palestina hasa hali mbaya ya Ukanda wa Ghaza katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC.
Mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni yanaendelea dhidi ya makazi ya raia katika Ukanda wa Ghaza kwa siku ya 25 mfululizo na takwimu za Wizara ya Afya ya Palestina zinasema kuwa azaidi ya awatu 8,000 wameshauawa shahidi ambapo nusu yao ni watoto madhlumu wasio na ulinzi wa Palestina.
Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, kikao cha 21 cha mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kimejadili ripoti ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC. Katika kikao hicho, mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika umoja huo amesisitiza kwa kusema: Ni jambo lisilo na shaka kwamba jinai zinazofanywa na Israel huko Ghaza, ni dhihirisho la wazi kabisa la jinai za kimataifa kwa vigezo vya mahakama ya ICC.
Siku chache zilizopita pia, Reza Najafi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya sheria za kimataifa alisema kuwa, mchakato wa kufuatilia jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Ghaza umeanza katika taasisi za kimataifa.
Jumamosi ya tarehe 7 Oktoba 2023, wanamapambano wa Palestina wakiongozwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya HAMAS walifanya operesheni ya kihistoria na ya kushtukiza ya #Kimbunga_cha_al-Aqsa na kutoa pigo kubwa la kijeshi, kijasusi na kiusalama kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Operesheni hiyo ya kishujaa ilifanywa na wanamapambano wa Palestina kujibu jinai za makumi ya miaka za Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.
Utawala pandikizi wa Israel ambao umeshindwa kupambana na wanamapambano wa Palestina kwenye medani ya mapambano, umeamua kufanya jinai kubwa kupindukia dhidi ya watoto, wanawake, vizee na watu wa kawaida huko Ghaza.