Abdollahian: Jitihada za kusitisha vita Gaza kwa njia za kisiasa zinaendelea
(last modified Thu, 02 Nov 2023 02:59:32 GMT )
Nov 02, 2023 02:59 UTC
  • Abdollahian: Jitihada za kusitisha vita Gaza kwa njia za kisiasa zinaendelea

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu na Qatar zinaendeleza juhudi za kisiasa za kutaka kusimamishwa vita kwa muda katika Ukanda wa Gaza haraka iwezekanavyo, huku utawala wa Kizayuni wa Israel ukiendelea kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika eneo hilo lililozingirwa.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo yake na waandishi wa habari baada ya kuhitimisha safari ya kiduru ya kuzitembelea Uturuki na Qatar kujadili kadhia ya Gaza na viongozi wa nchi hizo.

Amesema: Kuna mazungumzo yanayoendelea Qatar juu ya suala la usitishaji vita mara moja kwa misingi ya ubinadamu, ambao yumkini utapelekea kuingizwa na kusambazwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa, "Chini ya makubaliano hayo ya usitishaji vita, tutashuhudia mabadilishano ya wafungwa raia baina ya pande mbili, ikiwemo kuachiwa huru wafungwa wote wanawake wa Kipalestina." 

Aidha Amir-Abdollahian ameeleza bayana kuwa, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameafiki pendekezo la mwenzake wa Iran, Ebrahim Raisi  la kufanyika mkutano wa dharura wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kujadili mgogoro wa Gaza. 

Amir-Abdollahian (kushoto) na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki

Mauaji ya kimbari yanayoendelezwa na utawala haramu wa Israel  huko Ghaza  tokea Oktoba 7 yamesababisha vifo vya Wapalestina karibu 9,000 wakiwemo watoto zaidi ya 3,500 na wengine zaidi ya 23,200 kujeruhiwa. Aghalabu ya waliouawa katika hujuma hiyo ya Israel ni wanawake na watoto.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, juhudi za utawala wa Kizayuni wa Israel za kuingia Gaza kupitia ardhini ndani ya siku tatu zilizopita, hazijafua dafu.