Mkuu wa IRGC: Israel, Marekani zinakabiliwa na kinamasi huko Gaza
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Meja Jenerali Hossein Salami anasema vijana wa Kipalestina wanazoea hali halisi mpya huko Gaza, ambako Israel na Marekani zinakabiliwa na kinamasi.
Akizungumza Alhamisi mjini Isfahan, alisema vijana wa Palestina wanazoea hali mpya na wamejifunza sheria za vita. Wameibua kinamasi kwa Marekani na Israel sio tu kwenye medani ya vita bali pia katika siasa, ujasusi na usalama."
Ameongeza kuwa, Gaza itakuwa uwanja wa kuzikia Wazayuni. Walikuwa wakipigana ndani ya ngome na nyuma ya kuta na walidhani kwamba kuta hizo zitawalinda na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, lakini adhabu ya Mungu itawafikia kutoka mahali ambapo hawafikiri.
Aidha amesema: "Leo hii wamevuka kuta na kufichua vifaru vyao kwa vijana wa Kipalestina wanaowinda vifaru na mabuldoza kutoka karibu, kiasi kwamba vifaru vyao 180 kati ya 1,600 vimeharibiwa hadi sasa, ambayo ina maana zaidi ya asilimia 10 ya vifaru vimeangamizwa.”
Jenerali Salami amesema Israel lazima itarajie mshangao zaidi kama Kimbunga cha al-Aqsa ambayo ilishuhudia wapiganaji wa muqawama wa Palestina wakiteka maeneo yanayokaliwa kwa mabavu katika tukio moja kubwa zaidi katika historia ya Israel. Jenerali Salami ameongeza kwamba Waislamu wa dunia leo wanaunga mkono Palestina zaidi ya hapo awali na hata katika ulimwengu usio wa Kiislamu ulimwengu unasimama dhidi ya Marekani na washirika wake.
Wakati huo huo, Mkuu wa Kikosi cha Quds cha IRGC amelihakikishia tawi la kijeshi la Hamas katika Ukanda wa Gaza mshikamano wa Mhimili wa Muqawama na wapiganaji wa Palestina.
Mhimili wa Muqawama unajumuisha muungano kati ya Iran, Syria na makundi yanayoipinga Israel huko Lebanon, Iraq, Yemen na kwingineko ambayo yamelenga kwa makombora vituo vya kijeshi vya Israel na Marekani katika wiki za hivi karibuni katika kuonyesha mshikamano na Gaza.