"Utawala wa Kizayuni ndicho kielelezo kikuu cha uzushaji wa migogoro duniani"
Khatibu wa Salama ya Ijumaa ya leo ya hapa Tehran amezungumzia jinai za utawala wa Kizayuni kwenye Ukanda wa Ghaza na kusema kuwa, utawala unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu, ndicho kielelezo kikubwa zaidi cha kuzalisha migogoro kwenye eneo la Asia Magharibi na duniani kwa ujumla.
Jumamosi ya tarehe 7 Oktoba, 2023, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilitoa pigo kubwa la kihistoria kwa utawala wa Kizayuni, baada ya kuendesha uperesheni ya kishujaa ya #Kimbunga_cha_al-Aqsa dhidi ya Israel, kipigo ambacho hakiwezi kabisa kusahaulika katika historia.
Baada ya utawala wa Kizayuni kushindwa kukabiliana na wanamapambano wa Palestina umeamua kumalizia hamaki zake kwa watoto wachanga kwenye mahospitali ya Ghaza na dhidi ya watoto wadogo, wanawake, vizee na raia wa kawaida wa Palestina, jinai kubwa ambayo haijawahi kutokea mfano wake katika karne ya 21.
Shirika la habari la IRIB limemnukuu Hujjatul Islam Sayyid Mohammad-Hasan Abouturabi Fard, khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya Tehran akisema kwenye khutba za Sala hiyo kuwa, Palestina ni sehemu isiyotenganishika na mwili mmoja wa Uislamu. Ghaza nayo ni sehemu isiyotenganishika na ardhi nyigine za Palestina, hivyo ni wajibu wa kila Muislamu kuunga mkono ukombozi wa Palestina.
Amesema, kila mwenye hisia za utu na ubinadamu, lazima ataunga mkono mapambano ya Wapalestina mbele ya utawala katili wa Kizayuni unaomwaga damu za watoto wachanga kwa uungaji mkono kamili na wa pande zote za kisiasa, kijeshi na kiuchumi wa Marekani.
Hujjatul Islam Sayyid Mohammad-Hasan Abouturabi Fard ameashiria pia uchaguzi wa Bunge na Baraza la Wanachuoni Wataalamu la Iran uliopangwa kufanyika mwezi Machi mwaka 2024 na kusema kuwa, kujitokeza kwa wingi wananchi katika chaguzi hizo, kutazidi kuuimarisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuvunja njama za maadui wa taifa la Iran.