Mkuu wa IRGC: Israel imeshindwa, Wapalestina ndio washindi
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema utawala wa Kizayuni wa Israel umeshindwa na wapigania ukombozi (wanamuqawama) wa taifa la Palestina na kuwa utawala huo umeshindwa kutokana na makosa yake wenyewe.
Meja Jenerali Hossein Salami alisema Jumatatu kwamba Wazayuni wanatafuta ushindi bandia kwa kuwaangamiza watoto na pia kwa kuwashambulia kwa mabomu watu wote wanaodhulumiwa [wa Palestina] huko Ghaza. Ameongeza kuwa kila siku Wazayuni wanakabiliwa na mashambulizi ya wapigania ukombozi wa Palestina.
Kamanda Mkuu wa IRGC ameongeza kuwa, Wazayuni wamepanua operesheni zao katika Ukanda wa Ghaza na kujiweka wazi kwa njia ambayo ni rahisi kushambuliwa na wapiganaji wa Kiislamu ambapo matokeo yake ni kuwa "takriban vifaru 15 na magari mengi ya deraya huharibiwa kila siku sammbaa na askari wake kadhaa kuangamizwa."
Meja Jenerali Salami amesisitiza kuwa ulimwengu unabadilika na Uislamu unaenea duniani na kuongeza kuwa: "Mwenyezi Mungu akipenda, Wapalestina wataibuka washindi katika vita dhidi ya Israel."
Akiashiria mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wasio na hatia huko Gaza, Kamanda Mkuu wa IRGC amesema utawala wa Israel umeshindwa pia katika medani ya maadili, umetengwa kidiplomasia na umefanya ujinga katika mbinu zake.
A,esema matukio ya Gaza ya,efichua sera "zilizofichwa" za serikali za Magharibi na Wazayuni dhidi ya Waislamu. Kamanda Mkuu wa IRGC ameongeza kuwa vita vya Israel dhidi ya Gaza pia vimefichua sura halisi ya Marekani na washirika wake wanaodai kutetea haki za binadamu, uhuru, demokrasia, usalama na ustawi.
Amesisitiza kuwa Marekani, Israel na washirika wao walikuja katika eneo la Asia Magharibi kuzikalia kwa mabavu nchi za Kiislamu kwa kisingizio cha kukuza demokrasia, lakini wameua mamia ya maelfu ya Waislamu katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, wakaharibu miji mingi, na katika nchi kama vile Afghanistan , Iraq, Yemen, na Syria, magofu ya sera zao yamebakia.
Aidha Salami ameikosoa serikali ya Marekani kwa kuchochea migogoro mikubwa miongoni mwa mataifa ya Kiislamu na kuweka vizuizi katika Ukanda wa Gaza huku ikizuia kutekelezwa usitishaji vita.