Iran yazitaka nchi za Kiislamu zichukue hatua zaidi katika kuwaunga mkono Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i105262-iran_yazitaka_nchi_za_kiislamu_zichukue_hatua_zaidi_katika_kuwaunga_mkono_wapalestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema nchi za Kiislamu zinapaswa kuchukua hatua muhimu zaidi za kuwaunga mkono wananchi wa Palestina katika kukabiliana na ukatili wa utawala ghasibu wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 26, 2023 04:39 UTC
  • Iran yazitaka nchi za Kiislamu zichukue hatua zaidi katika kuwaunga mkono Wapalestina

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema nchi za Kiislamu zinapaswa kuchukua hatua muhimu zaidi za kuwaunga mkono wananchi wa Palestina katika kukabiliana na ukatili wa utawala ghasibu wa Israel.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran aliyasema hayo Jumamosi katika mazungumzo ya simu na Hakan Fidan Waziri mwenzake wa Uturuki.

Katika mazungumzo hayo, mawaziri hao wawili wa mambo ya nje walijadiliana kuhusiana na matukio ya hivi karibuni ya Palestina pamoja na masuala mengine yenye maslahi kwa nchi hizo mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema Iran na Uturuki, pamoja na nchi nyingine za Kiislamu, zinahitajika kuchukua hatua muhimu katika kuunga mkono taifa la Palestina.

Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa, ni lazima pia kuchukuliwe hatua madhubuti za kukomesha kikamilifu jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya taifa la Palestina katika Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Maoni yake yamekuja baada ya uvamizi wa hivi karibuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza uliopelekea kuuliwa shahidi karibu Wapalestina 15,000 kabla ya kuanza kutekelezwa siku ya Ijumaa mapatano ya usitishwa vita. Vita vya mauaji ya halaiki ya Israel dhidi ya Gaza vilianza tarehe 7 Oktoba baada ya makundi ya wanamuqama wa eneo hilo kuanzisha Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.

Maandamano ya kimataifa dhidi ya hujuma ya kinyama ya Israel Gaza

Utawala wa Israel pia unaendeleza uchokozi wake dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan tangu kuanza vita hivyo na kuua shahidi mamia ya Wapalestina katika eneo hilo linalokaliwa kwa mabavu.

Akirejelea suala la uhusiano wa pande mbili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza kuridhishwa na mwenendo unaoendelea wa uhusiano wa nchi hizo mbili katika nyanja zote.

Amir-Abdollahian ameelezea matumaini yake kwamba kuendelea kwa mashauriano ya kidiplomasia katika ngazi za juu kati ya Tehran na Ankara kutaimarisha na kuboresha zaidi ushirikiano wa pande mbili.

Kwa upande wake, mwanadiplomasia mkuu wa Uturuki amesisitiza azimio la Ankara la kufanyia kazi kurefushwa mapatano ya sasa ya Gaza.

Fidan ameutaja uhusiano wa nchi yake na Iran kuwa wa aina tofauti na wenye sura nyingi, akieleza imani yake kwamba kuendelea mashauriano na mikutano kati ya maafisa wa ngazi za juu wa pande hizi mbili kutapelekea kupanuka zaidi uhusiano wa pande mbili.