Kikao cha Kimataifa cha Soko la Mitaji ya Kiislamu chafanyika Tehran
Mkutano wa 15 wa Kimataifa wa Soko la Mitaji ya Kiislamu (ICM) unafanyika, Tehran, mji mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo unashirikisha wataalamu na wasimamizi wa ndani na nje ya nchi.
Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya Iran (SEO) na Jumuiya ya Mfumo wa Kifedha wa Kiislamu ya Iran, linalenga kutangaza suhula za kifedha za Kiislamu na kushughulikia changamoto na fursa zao.
Mkutano huo wa siku mbili ulizinduliwa Jumapili na Majid Eshghi, mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya Iran, ambaye aliwakaribisha waliohudhuria na kusisitiza umuhimu wa soko la mitaji la Kiislamu kwa maendeleo ya uchumi na jamii.
Mkutano huo unajadili mada mbalimbali zinazohusiana na soko la mitaji ya Kiislamu, kama vile utawala wa Shariah, dhamana za kifedha za Kiislamu, uwajibikaji kwa jamii, mfumo wa kifedha wa crypto, uwazi , suhula za muda mfupi za ufadhili, suhula za ufadhili wa pamoja na mahitaji ya kisheria na udhibiti.
Kwa mujibu wa waandaji, mkutano huo umevutia washiriki 42 kutoka Russia, Kuwait, Indonesia, Syria, Iraq, Pakistan, Maldives, Malaysia, Uturuki, India, pamoja na zaidi ya washiriki 200 wa Iran. Mkutano huo unatarajiwa kuwa jukwaa la kubadilishana mawazo na uzoefu, pamoja na kuimarisha ujuzi na utaalamu wa washiriki.