Nchi za dunia zataka kununua manuwari za kivita za Iran
Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, maendeleo ya jeshi la majini la Iran ni makubwa sana katika mikondo ya bahari kubwa duniani kiasi kwamba nchi mbalimbali zimeonesha hamu ya kununua manuari za Iran.
Kundi la 86 la manuwari za Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kisilamu ya Iran limerejea humu nchini baada ya kukata masafa ya kilomia 65,000 za baharini kuzunguka dunia na kusafiri kwenye bahari kubwa kama Bahari za Hindi, Pasifiki na Atlantiki. Wakati wa kuwasili humu nchini na kutia nanga huko Bandar Abbas, kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi ya kusini mwa Iran, kikosi hicho cha majini kimepokewa na kundi la vyombo mbalimbali vya baharini vya jeshi la Iran.
Shirika la habari la IRIB limemnukuu Admiral Shahram Irani, Kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu akisema kuwa, miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana kwenye safari hiyo ndefu ya baharini ni hamu iliyooneshwa na mataifa mbalimbali ya dunia ya kutaka kununua manuwari za Iran na kunufaika na maendeeleo makubwa ya Jamhuri ya Kiislamu katika uwanja huo.
Admiral Irani amesisitiza kuwa, mipango ya baadaye ya jeshi la Iran, ni kuongeza kwa kiwango kikubwa uwezo wa manuwari na vyombo vyake vya majini kutokana na maendeleo makubwa iliyonayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa katika masuala ya kiulinzi.
Kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pia kuwa, ujumbe wa safari hiyo ya kuzunguka dunia kupitia baharini ni wa urafiki kwa kila mpenda amani lakini pia ni onyo kwa maadui wa Jamhuri ya Kiislamu.
Amegusia pia kujiunga manuwari mpya ya Deylaman kwenye orodha ya meli za kivita za Iran jana Jumatatu na kuhimiza wajibu wa kushirikiana nchi jirani kulinda usalama wa maeneo yao.