Iran yaipongeza Yemen kwa kuwaunga mkono Wapalestina
(last modified Fri, 01 Dec 2023 03:21:55 GMT )
Dec 01, 2023 03:21 UTC
  • Iran yaipongeza Yemen kwa kuwaunga mkono Wapalestina

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amepongeza na kusifu uungaji mkono wa Yemen kwa taifa la Palestina, wakati huu ambapo utawala wa Kizayuni umeshadidisha jinai zake dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Hossein Amir-Abdollahian jana Alkhamisi aliutembelea ubalozi wa Yemen hapa mjini Tehran kwa madhumuni ya kufikisha shukrani za Jamhuri ya Kiislamu kwa San'a kwa hatua yake ya kuwaunga mkono na kuwatetea wananchi madhulumu wa Palestina. 

Katika mazungumzo yake na Ibrahim Mohammed al-Dailami, Balozi wa Yemen hapa mjini Tehran, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema, "Uungaji mkono wa Yemen kwa watu wa (Ukanda wa) Gaza na Ukingo wa Magharibi (wa Mto Jordan) unavutia."

Vikosi vya Yemen vimefanya operesheni kadhaa dhidi ya Israel, yakiwemo mashambulizi ya makombora ya balestiki na cruise mbali na kutwaa meli zisizopungua tatu za utawala wa Kizayuni, tangu utawala huo pandikizi uanzishe mashambulizi ya kinyama dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7.

Makombora ya Yemen

Zaidi ya watu 15,000 wakazi wa Ukanda wa Gaza wameuawa shahidi wakati wa mashambulizi ya anga ya Israel, na miongoni mwao kuna watoto wapatao 6,000.

Kabla ya hapo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alishukuru msimamo wa Musa Faki Mahamat, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika wa kulaani kushambuliwa kwa mabomu hospitali ya Al-Maamadani na utawala wa Kizayuni na kutoa wito wa kusitishwa mashambulizi mengine kama hayo na kutaka kutolewa misaada ya kibinadamu ya haraka kwa wananchi wanaokandamizwa wa Palestina.

Tags