Iran na Malaysia kushirikiana katika uchapishaji wa Qur'ani Tukufu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i105574-iran_na_malaysia_kushirikiana_katika_uchapishaji_wa_qur'ani_tukufu
Mwambata wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Malaysia amesema Jamhuri ya Kiislamu na Malaysia zitashirikiana katika uchapishaji wa nakala za kitabu kitakatifu cha Qur'ani.
(last modified 2023-12-03T23:30:20+00:00 )
Dec 03, 2023 23:30 UTC
  • Iran na Malaysia kushirikiana katika uchapishaji wa Qur'ani Tukufu

Mwambata wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Malaysia amesema Jamhuri ya Kiislamu na Malaysia zitashirikiana katika uchapishaji wa nakala za kitabu kitakatifu cha Qur'ani.

Habib Reza Arzani ameyasema hayo alipotembelea Wakfu wa Qur'ani wa Rasto mjini Kuala Lumpur na kusisitiza udharura wa kuwepo ushirikiano wa nchi hizo mbili katika kuchapisha nakala za Qur'ani Tukufu.

Amesema, hivi karibuni Iran na Malaysia zitaanzisha ushirikiano katika kuchapisha nakala za pamoja za Qur'ani. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wakfu wa Qur'ani wa Rasto amesema katika mkutano huo kwamba ujumbe wa Malaysia umetembelea na kukagua vituo muhimu vya kuchapisha nakala za Qur'ani Tukufu nchini Iran na kwamba pande mbili zimejadili na kuchunguza njia za kupanua ushirikiano katika uwanja huo.

Abdul Latif Mirasa pia amezungumzia vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika baadhi ya nchi za Ulaya na kusema: Katika wakfu huu tumeamua tutakuwa tukichapisha nakala milioni moja za Qur'ani na kuzipeleka katika nchi mbalimbali mkabala wa kila nakala moja ya Qur'ani inayochomwa moto katika nchi za Magharibi.