Rais Raisi: Mauaji ya halaiki ya Wapalestina yatapelekea kuangamia utawala wa Israel
Rais wa Iran Ebrahim Raisi amesema kuwa mauaji ya halaiki yanayotekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya wanawake na watoto wasio na hatia wa Kipalestina yatapelekea kuangamia utawala huo ghasibu.
Raisi aliyasema hayo jana Jumanne akizungumza katika Bunge la Iran huku vita vya kikatili vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza vikiwa vimesababisha vifo vya takriban Wapalestina 16,000, asilimia 70 kati yao wakiwa wanawake na watoto katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Amesema: "Ukatili dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Palestina ni chanzo cha majuto kwetu sote na ubinadamu." Aidha ameongeza kuwa: "Tunaamini kuwa kuuawa shahidi wanawake na watoto wa Kipalestina kutakomesha utawala bandia wa Kizayuni na tutashuhudia ushindi wa Wapalestina na pia kuangamizwa kwa Waisraeli."
Rais wa Iran pia alielezea kusikitishwa kwake na uungaji mkono unaotolewa na watu wanaojiita watetezi wa haki za binadamu, yaani Marekani na nchi za Magharibi, kwa mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya watu wa Palestina.
Halikadhalika amesema inasikitisha zaidi kwamba a taasisi za kimataifa, ambazo zina jukumu la kutetea wanyonge, haziwezi kutekeleza majukumu yao kutokana na mashinikizo ya madola ya kibeberu hasa Marekani.
Rais wa Iran hatahivyo aimeelezea matumaini kuwa wananchi wa mataifa ya dunia wameinuka kutetea haki za binadamu na utekelezaji wa haki na utaratibu mpya wa kutawala dunia.