Amir Abdollahian alaani mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni huko Ghaza
Hossein Amirabdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran siku ya Ijumaa alilaani mauaji ya halaiki yanayofanywa utawala wa Kizayuni huko katika Ukanda wa Ghaza katika mazungumzo ya simu aliyofanya na Annalena Baerbock, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani.
Hossein AmirAbdollahian huku akiashiria kuendelea mauaji ya kinyama ya wanawake na watoto huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, amesisitiza ulazima wa jamii ya kimataifa kulipa kipaumbele maalumu suala hilo muhimu linalohusiana na haki za binadamu.
Kuhusu uhusiano wa pande mbili, na sambamba na kuashiria uhusiano wa kiutamaduni na kihistoria uliopo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ujerumani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuheshimiana na kuzingatiwa maslahi ya pamoja ni muhimu katika kudumisha uhusiano katika nyuga mbalimbali. Ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha suala la kuboreshwa uhusiano wa Tehran na Berlin.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani pia ameashiria ulazima wa kusimamishwa mapigano huko Palestina na kuongeza kuwa mgogoro wa Gaza unaweza kutatuliwa tu kwa njia za kisiasa.
Huku akifafanua haja ya kuzingatiwa sheria za kimataifa zinazohusiana na haki za binadamu, Baerbock amesema: Ujerumani inaomba usaidizi wa Iran ili kupunguza mivutano katika eneo.
Katika mazungumzo hayo, pande mbili zimetilia mkazo umuhimu wa kushauriana ili kuimarisha ushirikianao wa nchi mbili na pia kujadili baadhi ya masuala ya kidiplomasia.