Ahmad Vahidi: Makundi ya kigaidi yanaungwa mkono na utawala wa Kizayuni
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran amesema kuwa, makundi ya kigaidi yanayotaka kuvuruga amani, usalama na umoja wa wananchi wa mkoa wa Sistan na Baluchistan nchini Iran yanaungwa mkono na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ahmad Vahidi, amesema hayo jana jioni alipowasili katika uwanja wa ndege wa Kanarak, kusini mwa mkoa wa Sistan na Baluchistan, ambapo aliwaambia waandishi wa habari kuwa, makundi ya kigaidi yanaungwa mkono na utawala wa Kizayuni na kuongeza kuwa, serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatarajia kutoka kwa nchi jirani ziwe umakini zaidi katika kudhibiti mipaka ya pamoja kwa sababu imedhihirika kuwa makundi ya kigaidi yametoka upande wa pili wa mpaka.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran amebainisha kwamba, serikali ya Pakistan inapaswa kudhibiti zaidi mipaka yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili kuzuia kupenya magaidi wanaotokea katika ardhi ya nchi hiyo.
Genge la kigaidi la Jaishul-Dhulm limekiri kuhusika na shambulizi hilo la kigaidi lililotokea kwenye makao ya jeshi la polisi la Rask, kusini mashariki mwa Iran Alkhamisi jioni ambapo watu 12 waliuawa shahidi katika shambulio hilo la kigaidi lililolenga makao ya jeshi la polisi huko Rask.
Ahmad Vahidi, amemtumia ujumbe Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu na kusema, magaidi na waungaji mkono wao watambue kuwa, mikono yenye nguvu ya vikosi vya ulinzi vya Iran kamwe haitoliacha shambulio hilo la kigaidi lipite vivi hivi bila ya kuadhibiwa magaidi na waungaji mkono wao.