Iravani: Kurefuka vita vya Gaza kunazidisha gharama za himaya Marekani kwa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i106108-iravani_kurefuka_vita_vya_gaza_kunazidisha_gharama_za_himaya_marekani_kwa_israel
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameionya serikali ya Joe Biden akisema: "Gharama za misaada na himaya ya Marekani kwa Israel zitaongezeka kwa kasi kutokana na kuendelea kwa vita na mashambulizi ya Israel Ukanda wa Gaza."
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Dec 17, 2023 08:00 UTC
  • Iravani: Kurefuka vita vya Gaza kunazidisha gharama za himaya Marekani kwa Israel

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameionya serikali ya Joe Biden akisema: "Gharama za misaada na himaya ya Marekani kwa Israel zitaongezeka kwa kasi kutokana na kuendelea kwa vita na mashambulizi ya Israel Ukanda wa Gaza."

Katika mahojiano yake na jarida la Marekani la Newsweek, Amir Saeid Iravani ameionya serikali ya Joe Biden kwamba, Israel haina uwezo wa kufanya uvamizi bila ya msaada na uungaji mkono usio na masharti wa Marekani na kusema: Gharama ya msaada na himaya hiyo ya Marekani inaongezeka kwa kasi kutokana na kurefuka vita vya Gaza.

Ameongeza kuwa: Marekani lazima ama iweke masharti na kupunguza uungaji mkono huo au iwe mhanga wa sera za kupenda makuu za watawala wa Israel.

Iravani amesema: "Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anaona maisha yake ya kisiasa katika kuendeleza vita vya Gaza, na Biden anakuona kuchaguliwa kwake tena kuwa kumo katika kumaliza vita vya Gaza. Mgongano huu wa maslahi hauwezi kudhibitiwa kwa kurefusha vita vya Gaza."

Benjamin Netanyahu na Biden

Akiendelea kujibu maswali ya Newsweek kuhusu athari za vita kati ya Israel na makundi ya wapigania uhuru wa Palestinana na matokeo yake kwa Iran, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu amesema: Suala muhimu zaidi kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuokoa maisha ya raia.

Amefafanua kuwa: Makundi ya Jihadi yamechagua njia ya mapambano na yameingia kwenye njia hii kwa uangalifu mkubwa na yamekubali kubeba gharama za mapambano hayo ya kupigania uhuru kwa ajili yao na familia zao, lakini watu wa kawaida, hasa wanawake na watoto, hawapaswi kuwa wahanga wa vita.

Iravani amesema: Muqawama na mapambano dhidi ya uvamizi ni utamaduni ambao sio tu kwamba hautapungua iwapo viongozi na mujahidina watauawa, lakini damu yao itaimarisha mapambano, na mujahidina zaidi watachagua njia ya Muqawama.

Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa: Kwa hakika Israel haiwezi kuiangamiza Hamas, lakini kwa mauaji ambayo imefanya, nguvu ya Muqawama itaimarika zaidi, ama kwa wapiganaji wapya wanaojiunga na Hamas au kwa kujitokeza makundi mapya katika medani ya mapambano ya ukombozi wa Palestina.