Iran yakosoa msimamo wa Russia kuhusu visiwa vitatu vya Jamhuri ya Kiislamu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Russia kwamba, Tehran haiwezi kufanya majadiliano na mashauriano yoyote juu ya mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya Jamhuri ya Kiislamu.
Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran jana Ijumaa alizungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Russia, Sergei Lavrov ambapo amekosoa vikali taarifa ya mkutano wa 6 wa Baraza la Ushirikiano wa Kiarabu na Russia huko Morocco kuhusu visiwa vitatu vinavyomilikiwa na Iran na kusisitiza kuwa, visiwa hivyo vya Bu Musa, Tomb Ndogo na Tomb Kubwa katika Ghuba ya Uajemi daima vitasalia kuwa milki ya Jamhuri ya Kiislamu.
Amesisitiza kuwa, visiwa hivyo vinavyopatikana katika maji ya Ghuba ya Uajemi ni milki ya daima ya Iran na ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza bayana kuwa, kutolewa taarifa kama hiyo ni kinyume na uhusiano wa kirafiki wa Iran na majirani zake.
Kwa upande wake, Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema Moscow daima inaheshimu mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya Iran.
Amesisitiza kuwa, Russia ina uhusiano wa kistratajia na Iran na kwamba sera ya Moscow ya kuheshimu mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya Iran haipasi kutiliwa shaka.
Mapema jana, Mshauri wa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa alilaani vikali taarifa ya Morocco na kusisitiza kuwa, nyaraka za historia zenye itibari ya kimataifa zinathibitisha kuwa, visiwa vitatu vya Bu Musa, Tomb Ndogo na Tomb Kubwa katika Ghuba ya Uajemi ni mali ya Iran.
Dakta Ali Akbar Velayati anasema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo inasisitiza suala la kuendelezwa sera ya ujirani mwema na kuheshimiana, inaamini kuwa ustawi na amani ya kanda hii ni jukumu la pamoja la nchi za eneo hili.