Iran yawanyonga majasusi wanne wa Mossad
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i106580-iran_yawanyonga_majasusi_wanne_wa_mossad
Majasusi wanne waliopatikana na hatia ya kushirikiana na shirika wa kutumia silaha, kutoa vitisho na kushambulia vikosi vya usalama katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Azarbaijan Magharibi wamenyongwa siku ya Ijumaa.
(last modified 2026-05-13T14:18:38+00:00 )
Dec 29, 2023 23:15 UTC
  • Iran yawanyonga majasusi wanne wa Mossad

Majasusi wanne waliopatikana na hatia ya kushirikiana na shirika wa kutumia silaha, kutoa vitisho na kushambulia vikosi vya usalama katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Azarbaijan Magharibi wamenyongwa siku ya Ijumaa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Mizan Online, ambayo ni kitengo cha habari cha Idara ya Mahakama ya Iran, wanne hao walikuwa sehemu ya kundi la watu kumi lenye uhusiano na Mossad, ambalo lengo lake kuu lilikuwa ni kuwabaini maafisa wa  usalama wa taifa  wa Iran waliokuwa wakivuruga njama za Israel dhidi ya Iran.

Majasusi wanne  wakuu wa timu hiyo, wakiwemo wanaume watatu na mwanamke, walinyongwa Ijumaa asubuhi baada ya kupatikana  na hatia ya kueneza "ufisadi katika ardhi" na "kupigana vita dhidi ya Mwenyezi Mungu kupitia ushirikiano wa kijasusi na Israel kwa nia ya kudhoofisha usalama wa Iran.

Wote walifuatiliwa na kukamatwa baada ya operesheni kali ya kiusalama  na ufuatiliaji wa karibu. Ripoti ya kukamatwa kwao ilichapishwa mnamo Oktoba 2022.

Mkuu wa Idara ya Mahakama mkoani Azerbaijan Magharibi Nasser Atabati amesema wanachama wa kikundi hicho, chini ya uangalizi wa moja kwa moja wa maafisa wa Mossad, walipewa maagizo ya kuwatafuta watu walio na uhusiano na vyombo vya usalama vya Iran na kupata habari kutoka kwao kupitia utekaji nyara, vitisho vya kuuawa, na mateso ya kikatili.

Aliongeza kuwa majasusi hao walionyongwa walipokea pesa kutoka kwa maajenti wa Israel na maafisa wa Mossad mara kadhaa kwa kazi waliyokamilisha.

Afisa huyo pia alibainisha kuwa majasusi waliwasiliana na maafisa wa Mossad kwa njia ya simu za video, na walifanya hujuma katika Mkoa wa Kaskazini Magharibi mwa Iran wa Azarbaijan, mji mkuu Tehran na Mkoa wa Hormozgan kusini mwa Iran.

Wanachama wa timu hiyo pia walichoma moto nyumba na magari ya watu wanaohusishwa na mashirika ya usalama ya Iran na pia walihusika hata katika majaribio kadhaa ya mauaji dhidi ya maafisa wa usalama wa Iran.