Iran yaipongeza Ansarullah ya Yemen kwa kuiunga mkono Palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameisifu na kuipongeza Harakati ya Ansarullah ya Yemen kwa kuwa na msimamo madhubuti katika kuwaunga mkono wananchi wa Palestina.
Hossein Amir-Abdollahian aidha amevipongeza vikosi vya Yemen kwa kuendelea kuwapa himaya wananchi madhulumu wa Palestina hasa wa Ukanda wa Gaza, ambao wanakabiliwa na jinai na mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel tokea Oktoba 7 mwaka uliomalizika wa 2023.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hayo katika mazungumzo yake na Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen, Muhammad Abdul-Salam ambaye yuko ziarani hapa mjini Tehran. Aidha amepongeza hatua zilizopigwa katika mazungumzo baina ya Yemen na Saudi Arabia.
Kwa upande wake, Msemaji wa Ansarullah, Muhammad Abdul-Salam ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uungaji mkono wake kwa mrengo wa muqawama, mbali na kumtaarifu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran kuhusu yalikofikia mazungumzo ya amani ya Yemen.
Vikosi vya ulinzi vya Yemen vimeapa kuendeleza mashambulizi yao hadi pale utawala katili wa Israel utakaposimamisha vita na kuondoa mzingiro ambao umeuwekea Ukanda wa Gaza kwa takriban miaka 17 sasa.
Wakati huo huo, Spika wa Bunge la Iran amesema himaya na uungaji mkono wa hali na mali wa Marekani kwa Israel ndio chanzo kikuu cha mauaji ya kimbari ya utawala huo katika Ukanda wa Gaza.
Mohammad Baqer Qalibaf amesema hayo katika mazungumzo yake na Msemaji wa Ansarullah, Muhammad Abdul-Salam hapa Tehran na kuongeza kuwa, hakuna shaka kuwa Marekani ndiyo inayobeba dhima ya vita vinavyoendelea Gaza.
Abdul-Salam ambaye pia ni Mkuu wa Timu ya Mazungumzo ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen kwa upande wake amebainisha kuwa, mashambulizi ya hivi karibuni ya Yemen dhidi ya meli za Israel katika Bahari Nyekundu ni onyesho la mshikamano na kusisitiza kuwa, wataendelea kupambana hadi ukombozi wa Palestina.