Spika: Shahidi Soleimani ni nembo ya umma wa Kiislamu
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) hakuwa tu shakhsia wa kidini na kitaifa wa Iran, lakini pia alikuwa nembo ya umma wa Kiislamu.
Mohammad Baqer Qalibaf alisema hayo jana Alkhamisi katika hotuba yake aliyoitoa kwenye Makaburi ya Mashahidi ya Tehran kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kutimia mwaka wa nne tangu kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani.
Qalibaf amesema moja ya mambo ambayo yalikuwa yanamshughulisha Jenerali Soleimani ni kuupeleka ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu katika pembe mbalimbali za dunia, na kuimarisha mrengo wa muqawama katika eneo la Asia Magharibi.
Amesema Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa dhidi ya utawala ghasibu wa Israel ni miongoni mwa matunda ya jitihada za Shahidi Qassem Soleimani.
Spika wa Bunge la Iran amesema operesheni hiyo ya Oktoba 7 mwaka uliomalizika ilikuwa ya aina yake na ambayo haijawahi kushuhudiwa dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika kipindi chote cha miaka 75 cha kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina.
Wakati huo huo, afisa huyo wa ngazi ya juu wa serikali ya Iran ameashiria mashambulizi ya kigaidi ya juzi Jumatano yaliyoua makumi ya watu katika mji wa Kerman kusini mashariki mwa Iran na kusema kuwa: Hujuma za kigaidi za namna hii kamwe haziwezi kulifanya taifa la Iran liache kuyaunga mkono makundi ya muqawama.
Kadhalika Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu katika hotuba yake hiyo, amerejelea msemo maarufu wa Shahidi Qassem Soleimani aliposema: "Sisi ni taifa la Imam Hussein", na kusisitiza kuwa, taifa ambalo linafuata njia ya Imam Hussein (AS) katu haliwezi kusalimu amri mkabala wa dhulma.
Mapema jana, Spika wa Bunge la Iran alifanya mazungumzo ya simu na Maspika wenzake wa nchi za Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu, Oman, Syria, Uturuki na Tunisia, ambapo walilaani vikali milipuko miwili ya kigaidi ilitokea katikati mwa umati mkubwa wa wananchi waliokuwa wakishiriki marasimu ya kumbukumbu ya kutimia mwaka wa nne tangu kuuawa shahidi Jenerali Soleimani huko Kerman, ambayo ilipelekea kuuawa shahidi makumi ya watu na kujeruhiwa mamia ya wengine.
Kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) limekiri kuhusika na shambulio hilo la kihaini ambalo limeendelea kulaaniwa katika kona mbalimbali za dunia.