IRGC: Shambulizi la kigaidi la Kerman limefeli kuyumbisha usalama Iran
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesema shambulio la kigaidi lililoua makumi ya watu katika mji wa Kerman wa kusini mashariki mwa Iran ni jaribio lililofeli la kutaka kuvuruga na kuyumbisha usalama hapa nchini.
Taarifa ya jana Alkhamisi ya IRGC imelaani shambulizi hilo la kigaidi na kueleza kuwa, hujuma hiyo imetokana na kinyongo cha maadui wa taifa la Iran hasa tabaka la vijana ambalo linamuheshimu na kumuenzi shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la SEPAH.
Miripuko miwili ya kigaidi ilitokea juzi Jumatano huko Kerman, kusini mashariki mwa Iran wakati watu walipokuwa kwenye kumbukumbu za mwaka wa nne wa kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la SEPAH. Miripuko hiyo iliyotokea karibu na kaburi la shahidi huyo mujahid iliua watu zaidi ya 80.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limebainisha kuwa, taifa la Iran litaendelea kufuata kwa nguvu zaidi njia ya shahidi Soleimani na kuzima njama na malengo yao batili ya maadui.
Taarifa ya jana Alkhamisi ya IRGC imesema shambulizi hilo la kigaidi na la kihaini limefichua kuwa maadui wameshindwa kufidia vipigo na hasara walizosababishiwa na Jenerali Soleimani.
Wakati huo huo, Jeshi la Iran limelaani miripuko hiyo miwili ya kigaidi huko Kerman iliyopelekea kuuawa shahidi raia wasio na hatia, wakiwemo wanawake na watoto wadogo.
Taarifa ya Jeshi la Iran imesema: Kitendo hiki cha kigaidi, kilichoua kundi la watu wasio na hatia, kimeonyesha dhati ya ukatili ya maadui wa Uislamu na mfumo wa Uislamu.