Raisi: Hujuma za Marekani dhidi ya Yemen zimefichua dhati yake ya shari
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya Yemen na kusema kuwa, hujuma hizo zimefichua dhati ya Washington ya kupenda shari, chokochoko na kukanyaga haki za binadamu.
Rais Raisi alisema hayo jana jioni katika mazungumzo yake ya simu na Mahdi al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen, ambaye taifa lake maskini la Kiarabu limekuwa mlengwa wa mashambulizi ya kinyama ya Marekani tangu Ijumaa iliyopita.
Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa, "Hakuna shaka kuwa, vitendo vya aina hiyo dhidi ya taifa ambalo limekuwa likipambana na uvamizi wa maajinabi kwa miaka mingi, na ambalo hivi sasa lina nafasi muhimu katika kuwalinda wananchi wa Palestina, havikubaliki na vinalaaniwa na mataifa yote huru duniani."
Rais wa Iran amebainisha kuwa, kuwauga mkono wananchi wasio na ulinzi wa Palestina ni msimamo madhubuti na usio tetereka wa Jamhuri ya Kiislamu.
Aidha Sayyid Ebrahim Raisi ameeleza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel hivi sasa unachukiwa na kulaaniwa katika kona zote za dunia kwa kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya raia wakazi wa Ukanda wa Gaza huko Palestina.
Kwa upande wake, Mahdi al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema wananchi wa Yemen wataendelea kuwaunga mkono na kuwapa himaya Wapalestina madhulumu wa Gaza.
Ameongeza kuwa, anataraji ulimwengu wa Kiislamu utatumia uwezo wake kuzuia jinai za kikatili zinazoendelea kufanywa na utawala haramu wa Israel na waitifaki wake.