Pakistan yatangaza kurejesha uhusiano kamili na Iran baada ya mivutano iliyojitokeza
Pakistan imetangaza kurejesha kikamilifu uhusiano wa kidiplomasia na Iran baada ya kujitokeza mivutano mikali ya mpakani ambayo haijawahi kushuhudiwa kati ya nchi mbili juu ya operesheni za kupambana na ugaidi.
Amesema Pakistan na Iran ni "nchi mbili ndugu ambazo kihistoria zimekuwa na uhusiano wa kiudugu na ushirikiano uliotawaliwa na heshima na upendo."
Mapema jana hiyohiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Jalil Abbas Jilani na mwenzake wa Iran Hossein Amir-Abdollahian walifanya mazungumzo kwa njia ya simu na kutoa wito wa kuwepo ushirikiano wa karibu katika nyanja mbalimbali ikiwemo kupambana na ugaidi na kuimarisha usalama mipakani.
"Jilani alionyesha utayari wa Pakistan kufanya kazi na Iran katika masuala yote kwa msingi wa moyo wa kuaminiana na kushirikiana," ilieleza taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan na kuongeza kuwa mwanadiplomasia huyo mkuu wa Islamabad "alisisitiza haja ya kuwepo ushirikiano wa karibu katika masuala ya usalama".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran naye pia alisema katika taarifa yake kwamba, mamlaka na umoja wa ardhi ya Pakistan ni jambo linalopewa umuhimu mkubwa na Iran na ni muhimu kwa nchi hizo mbili kushirikiana katika kuzima hujuma na kutokomeza kambi za magaidi zilizoko Pakistan.
Akiashiria operesheni ya hivi majuzi ya Iran dhidi ya kundi la kigaidi la Jaishul-Adl nchini Pakistan, Amir-Abdollahian alisema, operesheni hiyo ilifanywa ili kuzima tishio la shambulio la kigaidi lililokuwa likikaribia kutekelezwa.../